SIKU moja baada ya kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, kutoa ripoti ya uchunguzi wa mauaji ya mwanahabari, Daudi Mwangosi, huku ikikwama kuweka bayana kiini cha kifo hicho kutokana na kesi inayoendelea mahakamani, wasomi, wanaharakati, wanasiasa na wananchi wamepinga hatua hiyo.
Baadhi ya waliozungumza na gazeti hili waliiponda ripoti hiyo ya Kamati ya Dk. Nchimbi wakidai imeidhalilisha serikali na kuonesha mkanganyiko uliopo wa kujaribu kuwalinda polisi wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya raia.
Wadau hao pia walilisifu Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri (TEF) kutoka ripoti yao iliyojaa kila aina ya ukweli kuwa Mwangosi aliuawa na polisi kama picha za video na mnato zilizopigwa siku ya tukio zinavyojieleza wazi.
Wakati kamati ya Dk. Nchimbi katika uchunguzi wake ikidai kuwa nguvu iliyotumiwa na Jeshi la Polisi kutawanya wafuasi wa CHADEMA haikuwa sababu ya kifo cha mwanahabari huyo, wadau hao wameiponda wakisema ni aibu na kwamba hata wajumbe wake walionesha bayana kuwa walikuwa na aibu ya kuisoma.
Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azavery Lwaitama, alisema kuwa ripoti hizo mbili ni nzuri kwani kwa mtu mwenye akili zake timamu anaweza kuona jinsi serikali ya Tanzania ilivyofika mbali katika mambo ya ajabu.
“Waziri Nchimbi ni bora asingeitoa ripoti hiyo maana inajichanganya kwa sababu haina maelezo ya kutosha kuhusu kile alichoahidi mapema kuwa hatua zingechukuliwa baada ya kamati hiyo kumaliza uchunguzi wake,” alisema.
Alisema ripoti hiyo ni ya kijinga maana inaishia kauli tata za viongozi wasio na hatia badala ya kutaja bayana kuwa kiini cha mauaji hayo ni kuwazuia waandishi wa habari wasiwe wanaripoti mikutano ya CHADEMA na kuwadhibiti CHADEMA wenyewe.
Dk. Lwaitama alibainisha kuwa baada ya Waziri Nchimbi kupokea ripoti zote mbili, ni bora angekaa kimya na kuchukua hatua zaidi ya kuunda kamati nyingine ya kuwachunguza polisi.
“Polisi wameumbuka, maana hawakujua kama kuna picha zilikuwa zinapigwa na ripoti zote zimethibitisha ukweli kuwa lengo lilikuwa ni kuwazuia waandishi ili kuficha kile ambacho kingetokea kwa CHADEMA pale Nyololo,” alisisitiza.
Alishauri kuwa Waziri Nchimbi angejijengea heshima kubwa kama angejiegemeza kwenye ripoti ya MCT, lakini katika kulinda vigogo wa polisi wasiumbuliwe ndiyo maana ikaandaliwa ripoti ya kuwasafisha.
“Kama si Mwangosi basi angeuawa Dk. Slaa maana hata TBC1 walishaanza kupotosha kuwa alikuwepo eneo la tukio ili kuhalalisha mambo ya ajabu ambayo polisi wangeyafanya. Sasa baada ya kuona mlengwa hayupo wakamgeukia Mwangosi wakielewa kabisa amerekodi mipango yao yote,” alisema.
Dk. Lwaitama alifafanua kuwa kabla ya Mwangosi kuuawa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, alinukuliwa akimwambia kuwa ana kiherehere na askari mwingine akamwambia atakufa.
Alisema picha zinawaonesha watu saba wakimpiga Mwangosi na kisha kuuawa, lakini mahakamani kafikishwa mmoja tena anafichwa sura na kwamba Kamanda Kamuhanda bado hajaguswa wakati alishuhudia mpango mzima wa mauaji.
“Kuhangaika na ripoti ya Nchimbi ni kujipotezea muda, walifanya hivyo ili baadaye watoe sababu za kijinga za kupigwa na kitu chenye ncha kali, lakini picha zikawaumbua. Kama hawakuwa tayari kuyasema yaliyomo wangekaa na ripoti yao,” alisema.
Naye mwanaharakati Deus Kibamba, aliliambia gazeti hili kuwa ameisoma ripoti ya MCT, lakini ya Waziri Nchimbi hakuhangaika nayo kwani waliipinga tangu mwanzo wakijua si halali kisheria.
Alisema kuwa Waziri Nchimbi alikuwa mtuhumiwa katika tukio hilo, na hivyo hakuwa na mamlaka kisheria kuunda kamati hiyo na kuongeza kuwa wajumbe wa kamati hiyo licha ya kuheshimika sana kwenye jamii, lakini kwa ripoti hiyo wamejitia doa kubwa.
“
Watu wanakubali uteuzi kwenye tume na kamati hizo bila kuhoji maana wanatafuta maslahi kifedha. Kisheria Nchimbi hakupaswa kuunda kamati hiyo na hata MCT wao waliiunda kamati ya kimaadili si kisheria ndiyo maana tunaisifu ya kwao. Tulishasema tunahitaji tume ya kimahakama kuchunguza matukio haya wakatupinga,” alisema.
Watu wanakubali uteuzi kwenye tume na kamati hizo bila kuhoji maana wanatafuta maslahi kifedha. Kisheria Nchimbi hakupaswa kuunda kamati hiyo na hata MCT wao waliiunda kamati ya kimaadili si kisheria ndiyo maana tunaisifu ya kwao. Tulishasema tunahitaji tume ya kimahakama kuchunguza matukio haya wakatupinga,” alisema.
Alisema kuwa Jeshi la Polisi walikwishaonesha kupishana kwa kauli kutokana na tukio hilo, kwamba Waziri Nchimbi alisema hawatamshtaki mtu hadi kamati imalize kazi, lakini wakati ikiendelea askari mmoja alifikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Mtatiro Julius, alisema kuwa Nchimbi aliunda kamati ya kuendelea kujilinda yeye, serikali na CCM kwani kusema polisi hawakutumia nguvu kumuua Mwangosi si kweli.
“Mimi ukiachilia ripoti hizo nimetazama video ya mauaji hayo na inaonesha wazi kabisa kuwa polisi walimuua Mwangosi kwa makusudi kwa kutumia nguvu nyingi ambazo hazikuwa na sababu,” alisema.
Aliongeza kuwa ripoti ya Kamati ya Nchimbi ni ya kupikwa, kuwalinda polisi kwani hata kumshtaki askari mmoja ni mkakati wa kukwepa wengine wasijekutajwa wakawajibishwa.
Naye Katibu Mkuu wa chama kipya cha ADC, Limbu Kadawi, alisema kwa ujumla ripoti hiyo ni aibu kwa taifa na Nchimbi mwenyewe, kwamba hata Jaji Ihema wakati anaisoma alikuwa akiona aibu.
Alisema wakati umefika kwa wananchi kujifunza kukasirika wanapoletewa mambo ya kijinga na aibu kama hayo.
Kidawi alifafanua kuwa, hata waandishi walianza kugawanyika mapema tangu tukio hilo kutokea kwani katika maandamano yao pale Jangwani, baadhi walionekana kujikomba kwa Waziri Nchimbi wakati ndiye alikuwa akilaaniwa kwa askari wake kuua.
“Mauji ya Mwangosi yalikuwa wazi wala hayakuhitaji kamati hiyo kuchunguza maana askari wote walioonekana kwenye picha pamoja na kamanda wao Kamuhanda walipaswa kuwa wamekamatwa na kushtakiwa.
Habari na na Edson Kamukara
No comments:
Post a Comment