MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amekitikisa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa hatua yake ya kutangaza kuwania urais 2015, baada ya mwasisi wake, Edwin Mtei kumuonya kuwa hatua hiyo itasababisha mzozo na mpasuko ndani ya chama.Mtei alisema amekuwa akimshauri Zitto mara kwa mara kuhusu hatua yake hiyo akimtaka kuwaunganisha wana Chadema na siyo kuwagawa au kuwavuruga.
Kauli hiyo ya Mtei imekuja siku chache baada ya mbunge huyo kutangaza kwamba hana mpango wa kugombea ubunge mwaka 2015, badala yake anajipanga kuwania urais.
“Hakuna shida kuonyesha hisia, lakini unatengeneza mzozo mkubwa sana ukitangaza sasa. Mimi nimeshamshauri sana Zitto, ahakikishe anakiunganisha chama na siyo kukigawa wala kukivuruga,” alisema Mtei.
Mtei alisema hatua ya mbunge huyo kutangaza kutogombea tena ubunge na badala yake kujipanga kuwania urais mwaka 2015 umekuja mapema mno na kuonya kuwa itaibua mzozo ndani ya Chadema.
Mtei ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu enzi za utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, alisema kwamba wakati mwafaka ukiwadia, Chadema kitaamua ni nani mwenye sifa za kugombea urais akisema kina utaratibu wake wa kuwapata wagombea mbalimbali wa uongozi.
Alisisitiza kwamba siyo vibaya kwa Zitto kuonyesha hisia zake, lakini akasema kuwa ndani ya Chadema kwa sasa, kuna watu mbalimbali wanaopenda kuwania urais, lakini hawajatangaza.
“Dk Slaa (Willbrod) anataka, Freeman (Mbowe) anataka, Zitto anataka, hata mimi huenda nikataka kugombea. Hapa hakuna upendeleo, sifa ndizo zitakazoamua,” alisema.
Huku akimwagia sifa mbalimbali Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini, Mtei alisema kwa upande mwingine, Katiba ya Tanzania kwa sasa, inamnyima Zitto sifa za kuwania urais mwaka 2015 kwa kuwa hadi kufikia mwaka huo atakuwa amefikisha miaka 38, huku Katiba ikielekeza kuwa mgombea urais anatakiwa awe na miaka isiyopungua 40.
Alipoulizwa ya kwamba endapo uchaguzi mkuu ujao utafanyika huku Watanzania wakiwa na Katiba Mpya iliyopunguza umri wa kuwania urais, Mtei alisema endapo mbunge huyo atapambana kuhakikisha umri huo unapunguzwa, basi atakuwa ni mbinafsi wa kupindukia.
“Kama yeye akichukua hatua ya kupambana ili Katiba ibadilishwe kwa kuwa anataka kuwania urais, basi itaonekana ni mtu wa ajabu sana; ni mtu mbinafsi na siyo vizuri.”
Zitto apinga
Akizungumzia kauli hiyo ya Mtei, Zitto alisema: “Demokrasia haileti mizozo kwenye vyama vya siasa hata siku moja, bali humaliza mizozo. Udikteta, kuminya fikra huru na mawazo huru, ndivyo huleta mizozo kwenye vyama vya siasa.”
Alisema ni muhimu wazee wakawaacha vijana wawe huru kusema wanachofikiri kwa kuwa uhuru wa fikra na mawazo ni moja ya haki za msingi na moja ya nguzo za demokrasia.
“Namheshimu Mtei kama mmoja wa waasisi na mwenyekiti mwanzilishi wa chama. Chama chetu kimekua na kina uwezo wa kuhimili demokrasia ya ndani,” alisema Zitto akiongeza kuwa miaka 20 tangu kuanzishwa kwa vyama vingi, nchi inastahili kuimarisha vyama kidemokrasia.
“Ninarudia, nitaomba kupeperusha bendera ya chama changu kwenye uchaguzi wa urais mwaka 2015. Naamini kwamba ninaweza kuwezesha chama chetu kushinda na kuongoza dola na Chadema kutoa rais wakati baadhi ya waasisi wetu wakiwa hai na kuona vijana wao tunavyobadili maisha ya Watanzania na kutimiza ndoto zao,” alisema Zitto.
Alisema ana uwezo, uadilifu na uzalendo wa kutosha kuwa Amiri Jeshi Mkuu na kuunganisha Watanzania kuwa wamoja bila kujali rika, dini wala makabila yao... “Nimejiandaa kisaikolojia kukabili changamoto za ufukara wa nchi yetu.”
Septemba 26, mwaka huu Zitto alitangaza nia yake hiyo ya kuwania urais mwaka 2015, alipozungumza na wananchi katika mjadala ulioandaliwa na asasi ya kiraia ya Meza ya Duara uliofanyika maeneo ya Soko la Mwanga, mjini Kigoma na kuhudhuriwa na watu zaidi ya 200. Miongoni mwa maswali hayo lilihusu tetesi kwamba anataka kugombea urais katika uchaguzi ujao.
Katika majibu yake Zitto alisema: “Kwanza nataka niwahakikishie watu wa Kigoma msiwe wanyonge… mna uwezo wa kutoa rais wa nchi hii.
“Nimefanya kazi kubwa katika ubunge, nimeleta mabadiliko mengi kuanzia bungeni mpaka jimboni. Nadhani inatosha na hata nikiongezewa miaka mingine sitaweza kufanya yale yaliyonishinda katika kipindi cha miaka 10. “Kama Mungu ataniweka mpaka mwaka 2015, sitagombea ubunge tena kwa sababu kazi niliyofanya inatosha.Natangaza rasmi kuwa nitagombea urais kupitia chama changu cha Chadema, bila kusababisha msuguano wowote na sitaki kuingia katika historia ya kurudisha nyuma harakati za upinzani kushika dola.
“Nataka kuleta changamoto mpya, nitawaeleza watu wa chama changu nia hiyo na nitatoa hoja za msingi. Hata kama sitapata ridhaa yao, lakini huo ndiyo msimamo wangu. Iwapo chama kikiona sistahili au sifai, nitakubaliana na uamuzi huo. Watu wengi wanadhani urais ni cheo, hawajui kuwa ni nafasi ambayo inakufanya ufanye vitu ambavyo ni vikubwa na vya maendeleo kwa wananchi.
” Alipoulizwa kuwa mwaka 2015 atakuwa na miaka 39, hivyo kukosa sifa ya kugombea urais kwa mujibu wa Katiba alijibu: “Nadhani nina uwezo wa kuwa rais, sidhani kama Katiba inaweza kumzuia mtu mwenye uwezo asigombee na ndiyo maana ninaamini kuwa kipengele cha kuwa na miaka 40 kitabadilishwa katika Katiba Mpya.”Via www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment