VURUGU kubwa zimezuka leo Dar es Salaam baada ya kutokea mabishano yaliyoanza kama utani, baina ya WATOTO wawili, mmoja wa Kiislam na mwingine wa Kikristo, Emanuel Josephat (14).Watoto hao walikuwa wakibishana kuhusu imani na dini ambapo mtoto wa Kiislam alimwambia mwenzake kuwa, “Quran ni kitabu kitakatifu, endapo utafanya chochote kibaya juu yake basi utadhurika, utageuka kuwa nyoka au shura au unaweza kuwa kichaa”.
Hapo ndipo mtoto wa Kikristo alipoamua kuikojolea Quran ili kuona kama hayo yatatokea. Baada ya kitendo hicho, ndipo mwenziye alipopeleka taarifa kwa Mzazi wake na kisha suala hilo likawafikia waamini wa Kiislam kuwa, mtoto wa Kikristo ameikojolea Quran.Ghadhabu na hasira ziliwashika baadhi ya Waumini na kwenye majira ya saa 5 asubuhi, baadhi ya Waislamu walioghadhibika walikusanyika na kuivamia kituo cha Polisi cha Maturubai, Mbagala Kizuiani wakishinikiza kuachiwa kwa mtoto huyo ili wamuue.
Waamini hao ambao idadi yao inakadiriwa kufikia 3,000, baada ya kutawanywa na Polisi waliingia mitaani na kuchoma Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Mbagala Zakhem, wakaharibu Kanisa la Anglican, Wakavunja vioo katika kanisa la Wasabato, hali Knisa la Tanzania Assembly of God (TAG), Mbagala Kizuiani wakilichoma moto na kuchukua vifaa vya muziki na kuviunguza hadharani.
Vurugu hizo pia zimesababisha gari za polisi namba T142 AVV, PT 0966 na T 325 BQP, basi la UDA na gari la waandishi wa habari kutoka Clouds kuharibiwa kwa kupigwa na mawe na waandamanaji hao.Mkuu wa Polisi wa kikosi maalum kanda ya Dar es salaam, Kamanda Suleiman Kova amekiri kutokea kwa tukio hilo na uharibifu uliotajwa. Akasema kuwa tukio hilo lisiwekewe uzito wowote kwa sababu ni la kitoto na halikuwa na kusudi lolote ambalo watu wazima waliopaswa kulitafakari, wamejichukulia sheria mkononi.
Awali, waamini hao walikusanyika katika kituo hicho cha Polisi wakimtaka mtoto huyo ambaye alikuwa chini ya ulinzi aachiwe. Polisi walipogoma kufanya hivyo ndipo vurugu hizo zilipoanza.
Kikosi cha kutuliza ghasia kilionekana kuzidiwa nguvu na watu hao ambao walikuwa wakiwatawanya kutoka eneo moja wanakimbilia eneo lingine na kuleta madhara mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufunga barabara.
Hata hivyo, baada ya viongozi wa dini hiyo kufika wakiwa wameambatana na Sheikh wa Wilaya ya Temeke, Sheikh wa Taasisi na Jumuiya za Waislamu kukaa kikao na kamanda wa Polisi Wilaya ya Temeke, David Misime, walifikia muafaka wa kuwaita Waislamu hao na kuwatuliza lakini hali iliendelea kuwa si shwari kwani baada ya viongozi hao kuona waandamanaji hao wakikamatwa na kupigwa walikuja juu na kutishia kuondoka, “Ndio nini sasa sisi tupo hapa kwa kuleta suluhu lakini ili Waislamu watulie, lakini mnawapiga mbele yetu. Ndiyo nini sasa?” alihoji mmoja wao.
Baadhi ya magari yaliyoharibika katika maandamano ya waislam leo
Kwa upande wake, Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amewataka Waislam kuwa na busara kwa kuwa aliyefanya tukio hilo ni mmoja na sio kundi, hivyo si sahihi kuvunja na kuharibu mali za Kanisa kana kwamba Kanisa ndilo lililomtuma kufanya hivyo.
Akatolea mfano ambapo Mtume Mohammad S.A.W akiwa na watu wake Msikitini alitokea mtu mmoja akakojoa eneo la msikitini. Waumini walitaka kumvamia kwa hasira, lakini Mtume S.A.W aliwaambia wamwache amalize kukojoa kisha akawatuma wamwite na akaanza kumueleza sura ambazo zinafahamisha kuwa nyumba ya Mungu ni mahali patakatifu na hapafai kufanya kitendo kile. Sheikh akawataka Waislamu kuiga mfano wa Mtume S.A.W. na kuacha hasira; hasa ukizingatia aliyefanya kitendo hicho ni mtoto.
No comments:
Post a Comment