WANAFUNZI zaidi ya 700 katika Shule ya Msingi Mbambo, wilayani Rungwe wanajisaidia vichakani kutokana na shule hiyo kuwa na uhaba mkubwa wa matundu ya vyoo.
Tanzania Daima juzi ilitembelea shule hiyo na kushuhudia wanafunzi hao wakienda kujisaidia vichakani kutokana na shule kuwa idadi ndogo ya matundu ya choo.
Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini matundu manne kati ya matundu 12 ya vyoo vya shule hiyo ndiyo yanayofanya kazi wakati mengine yakiwa ni mabovu.
Kaimu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Boas Mwinyekule, alisema mahitaji ya vyoo katika shule hiyo ni matundu 29, lakini yaliyopo ni 12 ambayo hayawezi kukidhi mahitaji.
Akizungumzia tatizo hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Jonas Mwakyoma, alisema kwa sasa hakuna mpango wowote wa kuanza ujenzi wa vyoo shuleni hapo kwa kuwa hivi sasa wananchi wameelekeza nguvu zao kwenye ujenzi wa zahanati ya kijiji.
“Kwa sasa tunajenga zahanati ya kijiji, huwezi ukawayumbisha wananchi waache zahanati warudi kujenga vyoo, hawatatuelewa na matokeo yake wataanza kugoma. Tutaongeza matundu ya vyoo pindi tutakapomaliza ujenzi wa zahanati,” alisema mwenyekiti huyo.
No comments:
Post a Comment