Chama Cha Mapinduzi kinasikitishwa na kitendo cha kinyama alichofanyiwa Sheikh Fadhili Soraga cha kumwagiwa tindikali sehemu ya uso na kifuani. Sheikh Soraga ni mtu maarufu hapa Zanzibar kwani huwa anashiriki katika shughuli mbali mbali za kidini hapa nchini, yeye ni Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar. Sheikh Soraga amefanyiwa unyama huo na watu wasiojuulikana wakati akitoka kwenye mazowezi ya viungoasubuhi ya leo.
Sheikh Soraga ni miongoni mwa masheikh wachache hapa zanzibar wenye kuheshimika na kueleweka. Hivi karibuni Sheikh Soraga alitoa hutuba nzuri na fasaha kwenye sala ya Eid-Haji juu ya kuimarisha amani na utulivu katika visiwa vyetu vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Khutba hiyo aliitoa mbele ya viongozi wakubwa wakitaifa waliohudhuria katika sala hio, miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mh. Dk. Ali Mohamed Shein, Makamo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharifu Hamadi, Rais Mstaau wa awamu ya sita wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume .a viongozi wengine kadhaa.
Siku hiyo hiyo katika Baraza la Iddi lililofanyika katika Ukumbi wa Salama Bwawani Sheikh Soraga wakati akitoa khutba ya utangulizi aliwaasa tena wazanzibari na watanzania kwa ujumla juu ya umuhimu wa amani, lakini katika hafla hiyo Sheikh Soraga alikwenda mbali zaidi kwani alitoa takwimu za hasara iliyoipata Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano, mashirikaya watu binafsi na ya Umma, taasisi za Kidini pamoja na vyama vya Siasa hasa Chama Cha Mapinduzi kufuatia vurugu mbali mbali zilizokuwa zikifanywa na Uamsho.
Vitendo vya kumwagiwa watu tindikali hapa Zanzubar vimeanza siku nyingi. Kama tutakumbuka mnamo mwaka 1995 Kada wa Chama Cha Mapinduzi ndugu Ali Mwinyi Msuko alimwagiwa tindikali na watu wasiojuulikana huko Wete Pemba, mwaka 2007 wakati zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura huko Pemba Sheha mmoja alimwagiwa tindi kali, na mwaka uliopita Ndu. Rashid Ali Juma Mkurugenzi wa Baraza la Mji wa Zanzibar nae alimwagiwa tindikali na watu wasiojuulikana na leo hii Sheikh Fadhil Soraga Katibu wa Mufti Muu wa Zanzibar nae amemwagiwa tindikali pia na watu wasiojuulikana.
Chama Cha Mapinduzi kinasema kimechoka kusikia vitendo hivi vya kinyama vya kumwagiwa watu tindikali na watu wasiokuulikana. Tunaviomba vyombo vya Dola kuwatafuta watu hawa waovu wasio na huruma na wenzao ili wakamatwe waweze kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria, na kama Jeshi letu la Polisi uwezo wake ni mdogo wa kuuwafichua wahalifu hawa basi ni vyema wakaomba msaada kwenye vyombo vya upelelezi vya Kimataifa kama vile INTAPOL.
Mwisho Chama Cha Mapinduzi kinawaomba wananchi wote wapenda amani na utulivu kumuombea duwa Mwalimu wetu Sheikh Fadhil Soraga Mwenyezi Mungu ampe moyo wa subira yeye na familia yake na amjaalie wepesi ili apone haraka. Sheikh Soraga hivi sasa amesafirishwa kupelekwa Muhimbili kwa Matibabu zaidi.
“KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI’
MAPINDUZI DAIMA
Issa Haji Usssi Gavu
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC
Idara ya Itikadi na Uenezi
ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment