KATIKA mazingira ya kujihami baada ya kubanwa na Baraza la
Madiwani akitakiwa kufafanua kiasi cha fedha kitakachotumika kutekeleza
mradi wa ujenzi wa soko la kisasa mjini Bukoba, Meya wa Manispaa hiyo,
Dk. Anatory Amani, amelazimika kuibua tuhuma mpya akidai anahujumiwa.
Meya huyo ambaye ni Diwani wa Kata ya Kagondo (CCM), alitumia kikao
hicho cha Baraza la Madiwani kilichoketi juzi, kuibua tuhuma kwa baadhi
ya wanachama na viongozi wa chama hicho mbele ya Waziri wa Mali Asili na
Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, ambaye pia ni mbunge wa Bukoba Mjini.
Kikao hicho kilimbana Meya Amani kikitaka kujua mradi huo
utatekelezekaje kwa fedha kutoka vyanzo gani vya mapato na utagharimu
shilingi ngapi hadi kukamilika.
Hatua hiyo ilikuja baada ya wajumbe kumlalamikia meya huyo kuwa
amekuwa akifanya maauzi yote peke yake ikiwa ni pamoja na kusaini
mikataba kadhaa ya kutekeleza miradi pasipo kuwashirikisha madiwani.
Hata hivyo, katika hatua ya kushangaza, Dk. Amani ambaye alionekana
kujipanga mapema pamoja na wapambe wake, aligeuza kibao kwa ndugu wawili
wa Balozi Kagasheki, ambao ni Abdul Kagasheki na Abubakar Kagasheki.
Meya Amani alidai kuwa wanachama hao wa CCM wanawarubuni baadhi ya
wafanyabiashara mjini hapa kwa kuwashinikiza wajiorodheshe majina yao
na kisha kumfungulia kesi ya madai ya sh bilioni 5 kama fidia ya
kupisha ujenzi wa soko la kisasa utakaogharimu sh bilioni 12.
Katika kikako hicho ambacho Waziri Kagasheki akihudhuria kwa mara ya
kwanza tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka 2010, Meya Amani alisema
kuwa kuma kundi dogo wana-CCM na baadhi ya viongozi kama Abdul,
Abubakar na Mauled Kambuga, wanachochea ili ujenzi huo usifanyike.
Alidai kuwa anatolewa kafara kwa kushtakiwa yeye binafsi na si kama
meya, akitakiwa kulipa sh bilioni 5 kama fidia kwa wafanyabiashara wa
soko kuu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo inayosimamiwa na
chama chake na kuzingatia maazimio ya baraza la manispaa hiyo.
Dk. Amani alimweleza Waziri Kagasheki kuwa baraza hilo lina madiwani
wanaotokana na vyama vitatu vya CCM, CHADEMA na CUF lakini akabainisha
kuwa madiwani wa upinzani hawapingi mambo ya maendeleo bali wanaunga
mkono na kushirikiana na manispaa.
“Ninashtakiwa kuwa mimi si raia wa Tanzania bali wa Uganda, haya yote
ni kunitafuta na kukwamisha miradi ya maendeleo kwa mji wa Bukoba,”
alisema.
Akizungumza jana jioni kutoka mjini Bukoba, Waziri
Kagasheki alisema yeye kama mbunge wa Bukoba amesikitishwa sana na
kitendo cha meya kushindwa kujibu hoja na badala yake kuibua tuhuma
zisizo za msingi.
Kagasheki alisema kuwa miradi mingi jimboni humo inalalamikiwa na
wananchi kutokana na meya kutowashirikisha na kwamba hata baraza la
madiwani lilitaka awaeleze fedha za ujenzi wa soko zinapatikanaje.
“Inaonekana yako mambo mengi yanafanyika wananchi hawaelewi, sasa
tunapohoji fedha hizi za walipa kodi ni kwa nini tuingize mambo ambayo
ni tofauti na hoje lengwa. Jumamosi nitafanya mkutano na wananchi
nitawaeleza kila kitu,” alisema Waziri Kagasheki.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba ambaye pia ni Diwani wa Kata
ya Kashai, Yussuph Ngaiza, alitishia kumchukulia meya huyo hatua kwa
kukidhalilisha chama hadharani mbele ya wapinzani.
Akijibu tuhuma za meya kwa niaba ya wenzake, Abdul Kagasheki, alisema malalamiko hayo hayana ukweli wowote dhidi yao.
Kagasheki ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wazazi Mkoa wa Kagera, alisema
kuwa yeye pamoja na Maulid Kambuga ambaye ni Diwani wa Kata Kagya na
Abubakar Kagasheki, wamemfungulia kesi ya kashfa meya kutokana na
kuwatangaza kwamba wanataka kumuua.
Alifafanua kuwa hawahusiki na kesi ya wafanyabiashara wa sokoni
isipokuwa wakili anayewatetea wafanyabiashara hao ndiye anayewatetea pia
wao.
No comments:
Post a Comment