THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo Ijumaa Novemba 23, 2012 amepokea
taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Kampasi mbili za tiba ya afya
vinavyojengwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma na Mloganzila huko Kisarawe,
ambavyo pia vitatumika kama hospitali hapa nchini.
Kwanza Rais amepokea maendeleo ya ujenzi wa Kampasi ya Afya ya Chuo
Kikuu cha Dodoma kutoka kwa Mkurugenzi wa Mfuko wa Afya ya Jamii (National Health Insurance Fund) NHIF Bw. Emmanuel Humba.
Ujenzi wa kampasi hii umeshaanza na kufikia hatua ya juu na hospitali inatarajiwa kuanza shughuli zake rasmi mwaka 2015.
Kulingana na Bw. Humba, maandalizi ya kufanikisha uanzishaji wa Chuo/
Hospitali hiyo vimeshaanza ambapo baadhi ya wataalamu wakiwemo
Madaktari na watumishi wengine wako nchini na nje ya nchi kwa ajili ya
masomo na mafunzo mbalimbali.
Chuo hicho kinatarajia kuwa na vifaa vya kisasa vya tiba vinavyokidhi
mahitaji ya Afya na Elimu ya Udaktari wa kiwango cha Kimataifa.
Rais pia amepokea taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Kampasi ya
Mloganzila ambapo katika ujenzi na uanzishwaji wa Kampasi hizi zote,
Rais Kikwete amesimamia kuanzia hatua za awali.
Kampasi ya Mloganzila ambayo ni sehemu ya Hospitali kuu ya Muhimbili
inajengwa kwenye eneo la ekari 3800 na itakua sehemu ya kutolea mafunzo
kwa wanafunzi wa udaktari na huduma za Afya, lakini pia itakua sehemu ya
kutolea matibabu ya maradhi yote makuu na ya kawaida nchini.
Ujenzi wa Hospitali hii unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi
Januari, 2013 na unatarajiwa kukamilika miaka miwili baada ya ujenzi.
Katika hafla hiyo Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi
Muhimbili Prof. Ephata Kaaya ametumia nafasi hiyo kumkabidhi Rais
Kikwete Cheti cha Udaktari wa Public Health (Honoris Causa),
kufuatia Shahada aliyotunukiwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi
Shirikishi, Muhimbili Disemba, 2010 kwa Kutambua mchango wa Rais Kikwete
katika kuendeleza Sekta ya Afya nchini.
Akitoa taarifa hiyo ya maendeleo kwa Rais Kikwete, Prof. Kaaya
amesema tayari wataalamu na wafanyakazi wanaotarajiwa kufanya kazi
katika kampasi ya Mloganzila wameshaanza mafunzo. Mara hospitali hiyo
kubwa na ya kisasa itakapokamilika itakua na uwezo wa vitanda vya kulaza
wagonjwa mia sita (600).
Rais Kikwete amewapongeza wataalamu wote kwa juhudi zao na kuwa ahidi
kuwa lengo lake ni kuhakikisha nchi inaondokana na adha ya kupeleka
wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Rais amesema moja ya lengo kubwa la serikali yake, ni kutoa
kipaumbele katika sekta ya Afya ili kuhaklikisha watanzania wanapata
huduma bora, kupanua mafunzo ya Afya na kuongeza wataalamu watakaoweza
kutibu magonjwa yote makubwa hapa hapa nchini.
Rais amewaahidi watendaji wa Kampasi zote mbili kuwa atahakikisha
ujenzi wa huduma hizi muhimu kwa Umma haukwami kwa sababu ya ukosefu wa
pesa kwani ni jambo ambalo amedhamiria.
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu-DSM
23 Novemba, 2012
No comments:
Post a Comment