MKUU wa Wilaya ya Ukerewe, Mary Tesha, amepiga marufuku
biashara ya ngono katika wilaya hiyo hasa katika kambi za uvuvi, ili
kukabiliana na maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU).
Akihutubia wakazi wa mji wa Nansio juzi katika Uwanja wa Mongela
katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, alisema vitendo hivyo
vimekuwa chanzo kikubwa cha maambukizi ya VVU.
Alisema yeyote atayekwenda katika kambi za uvuvi bila shughuli
maalumu atakuwa anavunja sheria, hivyo anaweza kukamatwa kwa kosa la
uzururaji na kushtakiwa mahakamani.
Alisema katika uchunguzi wake wa muda mrefu amebaini baadhi ya
wanawake wanakwenda katika kambi hiyo kufanya biashara haramu ya
ngono, vitendo ambavyo mbali ya kukiuka maadili ya Mtanzania pia
ni chanzo kikuu cha maambukizi ya VVU.
Mkuu huyo wa wilaya alitoa kauli hiyo baada ya kupokea taarifa ya
hali ya maambukizi ya VVU iliyoandaliwa na Idara ya Maendeleo ya
Jamii ya Wilaya hiyo na kusomwa na Novatus Gabriel.
Katika taarifa hiyo pamoja na mambo mengine tatizo hilo limetajwa
kuwa sababu kubwa ya maambukizi mapya ya VVU katika wilaya hiyo.
Katika taarifa hiyo imeelezwa katika kipindi cha mwaka huu watu
wapatao 17,227 wamepima afya zao na kati yao 507 wamebainika
kuathiriwa na ugonjwa ambapo kati yao wanawake ni 316.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa katika kipindi cha mwaka huu wagonjwa
410 walioathirika wameongezeka na kuifanya idadi ya wagonjwa
wanaopewa dawa za kufubaza virusi vya ukimwi (ARVs) kufikia
2,209.
No comments:
Post a Comment