WAGANGA wawili wa kienyeji na washirika wao wamefikishwa katika
Mahakama ya Wilaya ya Bunda kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya
udanganyifu, baada ya kumtapeli mwalimu mmoja sh 620,000 kwa madai
kwamba wazizalishe ili ziwe nyingi zaidi.
Waliofikishwa katika mahakama hiyo mwishoni mwa wiki mbele ya Hakimu
Safina Simfukwe ni
Hussein Shaban na Revocatus Malima (30) ambao ni
waganga wa kienyeji.
Watuhumiwa wengine ni Nyamanga Chacha Mnanka (31), mkazi wa kijiji cha
Sabasaba wilaya ya Butiama na Magungu Fidelis (27), mkazi wa mtaa wa
Saranga mjini Bunda ambao wametajwa kuwa ni washirika wa waganga hao.
Mwendesha Mashtaka, Masoud Mohamed, alidai washtakiwa hao walitenda
kosa hilo Novemba 29, mwaka huu, majira ya mchana katika eneo la Stendi
Mpya mjini Bunda kwa kumtapeli mwalimu Margreth Alphonce wa Shule ya
Msingi Namhura.
Alidai kuwa baada ya kufanya utapeli huo walipanda ndani ya teksi na
mwalimu huyo hadi katika baa moja iliyoko mjini Bunda na kuanza kunywa
vinywaji, huku wakimwambia asubiri kidogo pesa zake ziweze kuzalishwa.
Alieleza kuwa watu hao walikamatwa na polisi baada ya raia wema kutoa taarifa, wakati wakijiandaa kumtoroka mwalimu huyo.
Washtakiwa wote walikana tuhuma hizo na wamepelekwa mahabusu baada ya
kushindwa masharti ya dhamana. Kesi itatajwa Desemba 14, mwaka huu.Habari na Ahmed Makongo, Bunda
No comments:
Post a Comment