Wahariri wanatoa maoni juu ya kuchaguliwa tena kwa Jacob Zuma kuwa Rais
wa chama cha ANC na pia juu ya aliyekuwa mbabe wa kivita katika Jamhuri
ya Kidemokrasi ya Kongo, Ngudjolo Chui
Kuhusu kuchaguliwa tena kwa Jacob Zuma na hivyo kuendelea kuwa Rais wa
chama tawala nchini Afrika Kusini, ANC, gazeti la "Süddeutsche" linasema
licha ya mwanasiasa huyo kuchaguliwa kwa kishindo, Afrika Kusini imo
katika mgogoro mkubwa. Mhariri wa gazeti hilo anasema sababu ya mgogoro
huo ni kashfa na udhaifu uliomo katika uongozi wa Zuma. Gazeti linasema
Afrika kusini ilikabiliwa na migomo iliyoandamana na umwagikaji wa damu.
Hali hiyo ilisababisha hasara katika uzalishaji na kuiathiri sekta ya
uchumi.
Gazeti la "Stuttgarter" linasema, chama cha ANC kinaweza kugawanyika katika siku za usoni kutokana na kushindwa kuzitimiza ahadi nyingi kilizozitoa kwa wafuasi wake.Mhariri wa gazeti hilo anafafanua kwa kusema mpaka sasa chama cha ANC bado kinaungwa mkono na mamilioni ya watu. Sababu ni kwamba kwa mamlioni ya waaafrika chama cha ANC kimeleta ukombozi. Lakini ahadi ambazo chama hicho kilizitoa kwa mamilioni ya wananchi bado hazijatekelezwa mpaka leo.
Watu wengi hawana ajira, na idadi yao inaongezeka,mfumo wa elimu kwa
ajili ya waafrika una mapungufu. Mamilioni ya waafrika wanaendelea
kuishi katika vitongoji vya masikini. Kwa hivyo kuchaguliwa tena kwa
Zuma kukiongoza chama cha ANC, kunaweza kusababisha mpasuko ndani ya
chama hicho.
"Mbabe wa kivita Ngudjolo Chui aachiwa"
Mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague ICC jana ilimwachia huru
,aliekuwa mbabe wa kivita Ngudjolo Chui aliefikishwa mbele ya mahakama
hiyo kujibu mashtaka ya kutenda uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa
kivita katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Lakini hakupatikana na
hatia.
Juu ya hukumu hiyo gazeti la "Neue Osnabrücker" linasema:"Jambo moja ni
la uhakika: uhalifu ulifanyika katika kijiji cha Bogoro mashariki mwa
Kongo. Watu waliuawa,wengine walichomwa moto wakati wakiwa hai, na
wanawake walibakwa. Lakini Ngudjolo Chui hakupatikana na hatia ya
mashtaka hayo" Gazeti la "Neue Osnabrücker " linasema hukumu hiyo
inathibitisha kwamba Mahakama ya mjini The Hague, ICC inafanya kazi yake
. Hatahivyo waendesha mashtaka wanayo haki ya kukata rufaa.
Mhariri wa "die tageszeitung" anakubaliana na mtazamo huo na anasema:
Mahakimu wa ICC wamebainisha kwamba mashtaka yaliyomkabili Chui yalikuwa
na mashaka-mashahidi wengi hawakuwa wazi katika kauli zao-walibabaika
na hawakuaminika. Katika hali hiyo mshtakiwa hawezi kutiwa hatiani.Ni
sahihi kabisa kwamba mahakimu wametoa haki pia kwa mbabe wa kivita.
CHANZO CHA HABARI NA IDHAA YA KISWAHILI DW.
No comments:
Post a Comment