SIKU moja baada ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni jijini
Dar es Salaam, Charles Kenyela, kutoa taarifa ya kumkingia kifua askari
wake anayetuhumiwa kumjeruhi mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania
Daima, Shaaban Matutu, mwanahabari huyo amefichua ukweli wa tukio zima.
Matutu ambaye aliruhusiwa jana mchana kutoka katika Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya kutolewa risasi hiyo
mwilini juzi, alisema kuwa unyama waliouonyesha polisi dhidi yake, kama
asingekuwa mwandishi basi huenda wangemfanyia kitu kibaya kupoteza
ushahidi.
Akizungumza jana muda mfupi baada ya kuruhusiwa, Matutu alifichua kuwa
taarifa aliyoitoa Kamanda Kenyella juzi kwa vyombo vya habari kuhusu
tukio hilo ni wazi imechakachuliwa, huku akionyesha hofu kwa raia
wasiokuwa na ndugu wa kufuatilia matukio ya jamaa zao haki zao
zinakuwaje.
Katika taarifa hiyo iliyowashangaza wananchi wengi wakiwemo majirani
zake Matutu walioshuhudia tukio hilo, Kenyela alisema kuwa katika
kuendeleza msako wa wahalifu, Desemba 4, mwaka huu, majira ya saa 3:30
huko Kunduchi Machimbo askari polisi namba F.8991 D/C Idrisa alijeruhiwa
kwa panga kwenye mkono.
Kwa mujibu wa Kenyella, askari huyo aliyejeruhiwa mkono wa kulia
alikuwa katika jitihada za kuwakamata watu waliokuwa kwenye nyumba ambao
walihifadhiwa wakituhumiwa kuwa majambazi.
“Askari huyo akiwa na wenzake wanne baada ya kujeruhiwa alirukiwa na
huyo aliyemkata panga (Matutu) na katika purukushani hizo risasi moja
ilifyatuka kutoka kwenye silaha hiyo aina ya bastola aliyokuwanayo
askari na kumjeruhi kwenye bega la kushoto mtu aliyekuwa akipambana
naye,” alisema.
Ndipo ilifahamika baadaye kuwa mtu aliyekuwa anapambana na askari ni
Shaban Matutu (30), mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima.
Kenyella aliongeza kuwa wote wawili mwandishi na askari walikimbizwa
Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu ingawa baadaye Matutu alipelekwa
Muhimbili kwa matibabu zaidi.
“Katika tukio hilo, askari wetu walifika kwenye nyumba hiyo kufuatia
taarifa kutoka kwa msiri kuwa katika nyumba ya mama J iliyokuwa Kunduchi
Machimbo kuna majambazi hatari. Ndipo Matutu alijitokeza na kumjeruhi
askari kwa panga na hatimaye naye pia akajeruhiwa kwa risasi,” alisema.
Taarifa hiyo ya Kenyella ilionekama kumshtua Matutu ambaye alilazimika kutoa ufafanuzi upya wa kile kilichotokea siku hiyo.
Akiwa ameshika ganda la risasi aliyofyatuliwa, Matutu alidai kuwa
alisikia mtu akigonga mlango na kumuita mkewe Mama J, wakati akimshauri
akafungue mlango alisikia tena sauti ya kiume ya mtu wa pili na hivyo
kutilia shaka watu hao.
“Nilichukua silaha ya jadi (panga) ili kujihami maana watu hao
walikuwa hawajajitambulisha, na nilimwamuru mke wangu akae upande wake
nami wangu kisha tukafungua mlango kidogo kuchungulia; baada ya kuona
kundi la watu, tukawa tunausukuma mlango kuufunga tena.
“Wakati tunajitahidi kuufunga, askari mmoja aliruka na kuupiga teke
kisha tukaanguka na mke wangu na tulipojaribu kuinuka askari mmoja
alinipiga risasi ya bega,” alisema.
“Sikujua kama ni mimi ndiye niliyepigwa risasi maana nilidhani ni mke
wangu ndiye kauawa lakini wakati nageuka nikaona damu zimetapakaa kwenye
shati langu, ndipo nikabaini kuwa aliyejeruhiwa ni mimi,” alisema.
Alisema kuwa alipandisha hasira na kuwahoji askari sababu ya kunipiga
risasi ndipo walijitambulisha kuwa wao ni askari na wanamsaka mtuhumiwa
Mama J.
“Nilimuuliza yule aliye nijeruhi kama mtuhumiwa ni yule mke wangu
aliyekuwa pale, akasema siye na hivyo nikarudia kumhoji ni kwa nini
wakanitendea hivyo. Ghafla walijidai kuanza kunihudumia
nilipowalazimisha wanipeleke hospitali,” alisema.
Ilifikia wakati askari huyo aliyemjeruhi kumlazimisha kuitoa risasi
hiyo mwilini kwa nguvu kwa njia ya kumbinya lakini alikataa uamuzi huo
akiona wanaweza kumuua.
“Tulikwenda kituo cha polisi Kunduchi Mtongani na kupewa fomu ya
matibabu (PF3) lakini niligoma kutolewa risasi pale na wakati wanazozana
wapi wanipeleke kuandika maelezo niliwaambia nimechoka wanipeleke
hospitali,” alisema.
Matutu anafichua kuwa salama yake ilikuja pale askari hao wakati
wanazozana, mmoja alimhoji mkewe akitaka kujua mumewe anafanya kazi
gani.
“Mama J aliwaambia ni mwandishi wa habari, wakauliza wa chombo gani,
akawajibu gazeti la Tanzania Daima, ndipo wakataharuki wakisema: “Toba
tumekwisha, itaandikwa hiyo!”
Matutu aliongeza kuwa baada ya majibu hayo walihamasishana waachane na
mpango wa kwenda kituo kingine kugonga muhuri fomu na badala yake
walimpeleka Mwanyamala.
“Tukiwa Mwananyamala baada ya madaktari kuniangalia na kunipa rufaa ya
kwenda Muhimbili, nilijiwa na hofu baada ya kuona askari aliyenipiga
risasi akiwa amefunga mkono wake kwa bandeji, nikataka nione kovu lake.
Matutu anasema katika hatua ya kushangaza, askari yule alifungua mkono
wake na hakuwa na jeraha la panga bali mchubuko kidogo na hivyo hata
daktari aliyekuwa akimhudumia aligoma kumtibu askari huyo akisema
hajaumizwa chochote.
“Tukiwa pale huku maaskari wakiwazuia baadhi ya wafanyakazi wenzangu
waliofika kuniona wasipige picha, askari walijaribu kila mbinu
kunishawishi nisifungue malalamiko dhidi yao na ndipo manesi waliokuwa
eneo hilo waliniambia nina bahati kwa vile nimeletwa nikiwa hai.
“Hapa tunaletewa watu wakiwa hoi au wamekufa na wanatupwa hapa kisha
askari wanaondoka halafu kesho unasikia majambazi wameuawa kwa risasi
wakipambana na polisi,” alisema.
Matutu alihoji kuwa ikiwa Kenyalla kasema kweli kwenye taarifa yake,
aeleze ni majambazi wangapi askari waliwakamata siku hiyo katika nyumba
yake, kwa nini hawakuondoka na panga linalodaiwa lilitumika kuwajeruhi
kama ushahidi? Polisi wanasaka watuhumiwa kwa kubomoa nyumba kwa mateke
bila uongozi wa serikali ya eneo husika?
“Huyo Mama J waliyekuwa wakimtafuta hata siku ile alikuwepo lakini
hawakumgusa licha ya kuwa tuhuma nyingi za kujihusidha na biashara
haramu, leo Kamanda anadiriki kupotosha ukweli wa tukio na kuniita raia
mwema jambazi?” alihoji.
Matutu alieleza kuwa hadi jana mchana walikuwa wamefika askari zaidi
ya watatu wakidai wametumwa na wakubwa zao ili kumshawishi alifungue
jalada la malalamiko kwa mdai kuwa uchunguzi unaendelea.
Matukio ya polisi kuua raia yamekuwa yakijirudia mara kwa mara nchini
lakini licha ya wadau kutaka iundwe Tume Huru ya Uchunguzi wa Kimahakama
ya mauaji hayo, serikali imekuwa ikikwepa na hivyo kuwapa polisi nafasi
ya kujichunguza na kutoa ripoti.
Taarifa zote za vifo vya raia waliopigwa risasi na polisi hazijawahi
kuwataja moja kwa moja wauaji badala yake wananchi huambiwa marehemu
aligongwa na kitu kizito chenye ncha kali akapoteza uhai.
Alipotafutwa tena jana, Kenyela aliendelea kushikilia msimamo wake
kuwa sababu za kujeruhiwa kwa mwandishi huyo zilitokana na kumpiga
askari kwa panga wakati wakiwa wanatekeleza wajibu wao.
Alisema taarifa walizopata kabla ya tukio hilo ni kwamba nyumba
aliyokuwa akiishi Matutu kuna majambazi, hivyo mwandishi hakuwa na
sababu ya kutoka na panga zaidi ya kujisalimisha na kujitambulisha kwa
asakri hao.
Kenyela alisema kutokana na tukio hilo kwa sasa wapo katika uchunguzi
na watakapobaini mkosaji ni nani katika kadhia hiyo watamchukulia hatua
zinazostahili.
Kuhusu mtuhumiwa Mama J aliyekuwa amefananishwa na mke wa Matutu
kutokana na kufanana kwa majina ya watoto wao, Kenyela alisema
wanamfuatilia na watakapompata atawajibika juu ya mwenendo uliosababisha
wananchi kumtilia shaka.
CHANZO CHA HABARI TANZANIA DAIMA.
No comments:
Post a Comment