WADAU wa huduma ya nishati ya umeme wamepinga maombi ya
Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) ya kuongeza bei kwa asilimia 155
kutoka wastani wa sh 141 kwa uniti moja.
Wakizungumza katika mkutano wa majadiliano ya kuongeza gharama za
umeme yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura)
yaliyofanyika katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam, wadau
hao walisema TANESCO imeshindwa kutoa huduma hiyo na kutaka kuingia
kwenye soko la kuangalia faida.
Akizungumza katika majadiliano hayo, mhadhiri msaidizi wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam Frateline Kashaga alisema kuwa wananchi wa vijijini
hawataweza kumudu gharama hizo kutokana hali ya uchumi inayowakabili.
Alisema kumekuwa na ongezeko la ugunduzi wa nishati za asili ambazo
alidhani zitapunguza gharama, lakini zinaongezeka huku akishangazwa na
Ewura kutumia mtaalamu kutoka Hispania ambaye hata na wenyewe pia
wameshindwa kutatua tatizo la umeme nchini kwao.
Naye Othuman Ramadhan, mkazi Temeke, alisema shirika hilo linataka
fedha za wananchi kwa kuongeza gharama huku likishindwa kutoa huduma
stahiki kwa wananchi.
Othuman alisema watendaji wa shirika hilo hususan wa Temeke
wametawaliwa na rushwa, hali inayowakandamiza wananchi wa hali ya chini.
“Ukienda kuomba kufungiwa huduma ya LUKU unaambiwa gari haina
mafuta, mkiwa wengi mnaambiwa mchangie fedha ya mafuta lakini
mkishachanga gari haipitii kituo cha mafuta sasa hayo mafuta sijui
yanatoka wapi?” alihoji Othuman.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO, Felchesmi Mramba,
alisema wametoa ombi hilo kutokana na ongezeko la gharama za kuendesha
shirika ambazo zinapanda mara kwa mara.
No comments:
Post a Comment