JESHI la Polisi mkoani Singida, limefanikiwa kuwakamata watu 25
wanaotuhumiwa kuwa majambazi wakiwa na vitu vilivyoporwa kwenye gari la
wafiwa lililokuwa limebeba maiti ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo
cha Sokoine (SUA) kwenda Tarime mkoani Mara.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida (ACP), Linus Sinzumwa, alisema kuwa
watuhumiwa hao wamekamatwa jana kufuatia msako mkali ulioendeshwa na
askari polisi kwa kushirikiana na wananchi.
Alisema kuwa watuhumiwa hao wamekutwa na vitu mbalimbali walivyopora
usiku wa kuamkia Jumamosi ya wiki iliyopita katika eneo la Kindai
Manispaa ya Singida.
Sinzumwa alitaja mali zilizokamatwa kuwa ni pamoja na nguo za
wasindikizaji, kadi mbili za ATM za CRDB, chaja mbili za simu,
vitambulisho vya wafanyakazi hao, kamera, Laptop, simu, pamoja na sh
20,500 zizookotwa eneo la tukio.
Aliongeza kuwa pia watuhumiwa hao walikutwa na rungu nne na fimbo
kadhaa vilivyotumika katika kuwapiga wafanyakazi hao wa SUA kabla ya
kuwapora fedha sh milioni 10, simu za mkononi na mali zingine.
Kamanda alifafanua kuwa polisi bado wanaendelea kuwahoji watuhumiwa
hao ili kubaini vinara wa tukio hilo kwani baadhi yao walikuwa
wakijitapa kwenye vijiwe vya pombe kuwa na fedha za matumizi , huku
wengine wakidai wanakula fedha za jeneza.
“Kwa sasa majina hatuwezi kuyataja maana bado tunaendelea na upelelezi
na kuwasaka wengine na baadaye tutafanya upembuzi ili kuwabaini wale
wahusika lakini pia nawaomba hawa wenzetu wa Tanroads kutoa mawe makubwa
ambayo yapo pembezoni mwa barabara, ambayo wahalifu wanayatumia kuteka
magari,” alisema.
Mwishoni mwa wiki iliyopita kundi la majambazi zaidi ya 10 yaliteka
gari la SUA lililokuwa limebeba mwili wa marehemu mwanafunzi wa chuo na
kupora fedha, simu za mikononi na vitu vingine kisha kuvunja jeneza na
kumpekua marehemu.
Gari hilo aina ya Land Cruiser hard Top lenye namba za usajili SU
37012 lilikuwa likitotokea Morogoro kupeleka msiba wa mwanafunzi wa
mwaka wa tatu Munchari Lyoba aliyefariki chuoni hapo, ambaye ni mkazi wa
Tarime, mkoani Mara.
No comments:
Post a Comment