MGOGORO mkubwa unaoendelea kufukuta ndani ya Chama cha Mapinduzi
(CCM) Wilaya ya Bukoba Mjini mkoni Kagera kati ya madiwani na Meya wa
Manispaa hiyo, Anatory Amani, umemlazimu Makamu Mwenyekiti wa chama
hicho, Philip Mangula, kwenda kutuliza upepo.
Kiongozi huyo anatarajiwa kuwasili mjini Bukoba leo kujaribu kutafuta
muafaka wa kutuliza fukuto la madiwani hao kutaka kumng’oa Amani,
wakimtuhumu kuwa ameingiza halmashauri kwenye miradi ya kifisadi.
Baadhi ya madiwani hao tayari wameapa kuwa wako radhi kupoteza
nyadhifa zao au kwa kufukuzwa au kujivua uanachama lakini lazima
wahakikishe Amani anang’oka ili kuinusuru CCM katika tuhuma za ufisadi.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka mjini Bukoba, zinasema kuwa
CCM imelazimika kumtuma Mangula baada ya Amani kukimbia kikao cha
madiwani wa chama hicho kilichokuwa kimjadili ili kutafuta ufumbuzi wiki
iliyopita.
Meya alitumia sababu ya ugonjwa na kuondoka kikaoni muda mfupi baada
ya katibu wa kikao, Ashura Hassan na msaidizi wake, Hilde Blandus, nao
kuondoka kwa visingizio kama hivyo.
Pamoja na kudai kuugua, Amani aligoma kuwapatia wajumbe muhtasari wa
kikao cha kamati ya siasa ya wilaya kilichopita akidai katibu wake
aliondoka nazo.
Meya huyo ambaye pia ni diwani wa kata ya Kagondo, anadaiwa kutumia
vibaya madaraka yake kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu na hivyo
kikao hicho cha madiwani wa CCM kilikuwa kijadili na kupata muafaka wa
ama ang’oke mwenywe au asubiri kura za kikao cha Baraza la Madiwani
kilichokuwa kiitishwe leo.
“Kikao hicho kilikuwa kijadili na kisha kupeleka ripoti kwenye kamati
ya saisa ya wilaya, lakini kutokana na kuahirishwa bila muafaka ina
maana madiwani tunaendelea na hoja yetu kwenye ‘full council’,” alisema
mmoja wa madiwani hao.
Tayari madiwani nane wa CCM akiwemo Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi
Khamis Kagasheki, na wengine wawili wa upinzani wametia saini hati ya
kumtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo, aitishe kikao cha dharura ili
kumng’oa meya huyo.
Hata hivyo, kikao cha Baraza la Madiwani kilichokuwa kiitishwe leo
hakitakuwepo kwa kile kilichodaiwa kuwa Amani kupitia mwanasheria wake
alimwagiza mkurugenzi asikiitishe akidai madiwani hao walikiuka kanuni.
Kaimu mkurugenzi wa manispaa hiyo, Salapion Rujugulo, alikanusha madai
hayo jana, akisema kuwa mkurugenzi alikuwa nje ya kituo akifanya
mitihani yake chuoni Mzumbe, kwamba akirejea atawaandikia barua madiwani
kuwaalika kikaoni.
Licha ya tarehe ya kikao kutotajwa, Tanzania Daima ilidokezwa kuwa
mkurugenzi huyo, Hamis Kaputa, jana alikuwa njiani kurudi kazini
kumuwahi Mangula ambaye anaingia mjini humo akitokea Mwanza.
Hoja ya kumng’oa meya iliibuliwa hivi karibuni na Balozi Kagasheki,
ambaye pia ni Waziri wa Malialisili na Utalii, akiunga mkono msimamo wa
CHADEMA, kupinga miradi ya uuzwaji wa viwanja zaidi ya 5000 na ujenzi wa
soko la kisasa.
Kagasheki aliapa mbele ya wapigakura wake kuwa hayuko tayari kusutwa
na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, kutokana na mikataba ya
siri yenye harufu ya kifisadi aliyoisaini Amani kwa kificho bila
kuwashirikisha madiwani wenzake.
Taarifa za ndani zinadai kuwa rushwa imeanza kutembezwa kwa baadhi ya
madiwani wa vyama vyote ili kuwarubuni wasipige kura ya kumng’oa meya.
Baadhi ya vigogo wa serikali akiwemo mkuu wa wilaya na mkoa,
mwenyekiti na katibu na chama tawala mkoa wa Kagera, wamekuwa wakifanya
kila juhudi kumnusuru Amani asing’olewe.
Mkuu wa Mkoa, Kanali mstaafu Fabiani Massawe, ametajwa kumkingia kifua
meya kwa kuwaziba midomo madiwani wasichukue uamuzi wao, jambo ambalo
limeibua mgawanyiko kwa baadhi ya wana-CCM mkoani humo wakihoji ni kwa
nini anamlinda mtuhumiwa.
Mgogoro huo ulikwishamfikia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na Kanali
Massawe anadaiwa kujaribu kutaka kumshawishi Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia, aingilie kati.
“Massawe anahaha kumnusuru meya lakini sisi tunaangalia salama ya
chama chetu mbele ya upinzani kwenye uchaguzi ujao. Huyu alijaribu
kumpigia simu Ghasia lakini waziri huyo alimtaka ampelekee malalamiko
kwa maandishi akisema hafanyi kazi kupitia simu,” alisema.
Halmashauri hiyo ina madiwani 24, watatu wa CUF, wanne wa CHADEMA na 17 wa CCM.
Ili kupitisha uamuzi huo wa kumuondoa meya, ni lazima robo tatu ya madiwani yaani 16, wapige kura ya kuunga mkono hoja hiyo.
Miongoni mwa vigogo waliosaini hati ya kutaka kuitishwa kikao cha
kumng’oa meya huyo ni Naibu wake, Alexander Ngalinda (Diwani wa Kata ya
Buhende), na Yusuf Ngaiza (Kashai) ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM
Manispaa ya Bukoba.
VIA TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment