SIKU chache baada ya wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha
(IFM) kufanya maandamano, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Suleman Kova, amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke,
Englbert Kiondo, kusimamia usalama wa hosteli za wanafunzi hao zilizoko
Kigamboni.
Akizungumza jana, Kova alisema
amelazimika kutoa agizo hilo baada ya kuwepo kwa mvutano kati ya Kiondo
na wanafunzi hao ambao walidai taarifa zote za uhalifu walizofanyiwa na
kundi la vibaka kwenye hosteli zao zimeripotiwa katika kituo kidogo cha
polisi Kigamboni.
Naye msimamizi wa hosteli mojawapo, aliyefahamika kwa jina la Sanfroza
alieleza wazi kuwa anashangazwa na ripoti ya polisi kuwa matukio ya
vitendo hivyo hayako katika orodha kwa sababu yote yameripotiwa
ipasavyo.
“Tunachotaka sisi kwa sasa ni jeshi la polisi kuwajibika katika
vitendo vyote vya uhalifu vilivyotokea hosteli, kwa sababu majina ya
vibaka wote yameripotiwa polisi Kigamboni, iweje leo warushiane mpira
wenyewe kwa wenyewe?” alihoji Sanfroza.
Wanafunzi hao walifanya maandamano Januari 14, mwaka huu, ambapo
Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kiliingilia kati kwa kuwatawanya kwa
mabomu ya machozi.
Pamoja na hilo, Kova aliahidi kutoa ufafanuzi wa matukio hayo wakiwemo
vibaka waliohusika wawe ndani ya Dar es Salaam au nje ifikapo Januari
30, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment