UONGOZI wa mbingwa wa Kombe la Kagame, Yanga, umemtema daktari wake,
Juma Sufiani,kwa kushindwa kuambatana na timu nchini Uturuki.
Yanga iliondoka nchini Desemba 30, kwenda Uturuki kwa kambi ya wiki
mbili na bila kutarajiwa uongozi ulishangaa Dk. Sufiani kushindwa
kutokea uwanja wa ndege wa kimataifa Julius Nyerere (JNIA).
Awali, uongozi kumtaka daktari huyo kuandika barua ya kujieleza, sababu zilizomfanya kutotokea siku timu inaondoka.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa sharti la kutotajwa jina
kwa sasa, mmoja wa viongozi wa klabu hiyo alisema kwa kitendo hicho
ambacho ni kinyume cha taaluma, uongozi unatarajia kumnyang’ang’anya
kibarua hicho na kumpa anayetambua wajibu na kazi yake.
“Kitendo cha timu kuondoka bila ya daktari, hata sisi viongozi
kilitukera sana na ndiyo maana tukamtaka ajieleze kabla uongozi
hamjamchukulia hatua zaidi,” kilisema chanzo hicho cha uhakika kutoka
ndani ya klabu hiyo kongwe hapa nchini.
Aidha, kiongozi huyo alisema licha ya Dk. Sufiani kujitetea kwa
maandishi, lakini uongozi haujaridhika, hivyo atavuliwa majukumu hayo.
Ilielezwa kuwa, kitendo cha Dk. Sufiani kushindwa kuondoka na timu,
kulisababisha kadhia kwa wachezaji hususan Frank Domayo aliyeumwa
malaria na Hamis Kiiza kifundo cha mguu, ambapo ilibidi kuomba msaada wa
madaktari wa Hoteli ya Fame Residence, ambao waliwatibu na kupona.
Sufiani amefungashiwa virago ikiwa ni takriban miezi mitano tangu
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu na Katibu Mkuu, Selestine
Mwesigwa ‘Koffi Anan’ nao kupewa mkono wa kwa heri.
Awali, Dk. Sufiani alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi kwanini
hakuambatana na timu, alidai uongozi wa Yanga unazijua na tayari
ameishawafahamisha.
Lakini juhudi za kumsaka jana ili athibitishe kama amepata barua ya
kuondolewa katika kibarua chake hazikuzaa matunda kwani hakuweza
kupatikana kupitia simu yake ya kiganjani.
No comments:
Post a Comment