JESHI la Polisi nchini kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) wamesema kuanzia Aprili mosi mwaka huu watazifuta leseni
zote za zamani na madereva watapaswa kuomba upya.
Zoezi la kubadili leseni za kuendesha magari ya aina zote litakamilika Machi 31, mwaka huu.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mnadhimu Kikosi cha
Usalama Barabarani, Johansen Kahatano, alisema hadi kufikia Desemba 31,
mwaka jana, leseni 616,349 ndizo zilizokuwa zimetolewa nchi nzima.
Alisema takwimu hizo za leseni haziendani na idadi ya vyombo vya moto
vilivyosajiliwa na
TRA ambapo hadi kufikia Desemba mwaka jana vilifikia
1,164,574 hali inayoonesha kuwepo na madereva wasiokuwa na leseni
halali.
“Kazi ya utoaji leseni mpya ilianza Oktoba mosi, 2010 na itakamilika
Machi 31, mwaka huu na atakayeshindwa kubadili ya zamani atatakiwa
kuomba upya na kuingia katika mafunzo ya ‘learners’ na atakayeendesha
gari bila leseni, atakamatwa na kufikishwa mahakamani,” alisema.
Kahatano alisema lengo la kuanzishwa mfumo huo ni kuinua kiwango cha
udereva kupitia mafunzo ya lazima hususan madereva wa mabasi yanayobeba
abiria.
Pia alisema kuwa itasaidia kuondoa tatizo la kughushi na kudhibiti
mienendo ya madereva kupitia kumbukumbu za makosa zitakazotunzwa kwenye
leseni ya dereva.
Kahatano alieleza kuwa zoezi la kukagua leseni litafanyika nchi nzima
kuanzia Aprili mosi mwaka huu na kuwaagiza madereva kutembea na leseni
zao ili kuepuka usumbufu.
Habari na Happiness Mnale-Tanzania Daima.
Habari na Happiness Mnale-Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment