KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibrod Slaa, leo anatarajiwa kufungua kongamano la wanafunzi wa vyuo
vikuu vilivyoko Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa Muungano wa Wanafunzi wa
CHADEMA Vyuo Vikuu (CHASO) mkoani Dar es Salaam, Freddy Chacha alisema
kongamano hilo litafanyika katika Ukumbi wa Msimbazi Center.
Alisema katika kongamano hilo, vijana wanatarajiwa kuwaapisha viongozi
wa shirikisho hilo kwa Mkoa wa Dar es Salaam, kueleza mipango mipya
kuelekea mwaka 2015, kutambulisha matawi na viongozi wake kwa viongozi
wa kitaifa.
Pia kuandikisha wanachama wapya na kutoa tamko lao dhidi ya vijana
waliofanya usaliti, na kuanza kuichafua Chaso kwa kueneza harakati mbaya
za CCM dhidi ya CHADEMA.
Mwenyekiti huyo alisema pamoja na Dk. Slaa, viongozi wengine wa chama
hicho wanaotarajiwa kuwepo ni Mbunge wa Ubungo, John Mnyika; Mbunge wa
Arusha Mjini, Godbless Lema; Mwenyekiti wa BAVICHAf Taifa, John Heche;
Mhadhiri wa Chuo Kikuu na Mkuu wa Kitivo cha Elimu katika Chuo Kikuu
kishiriki cha Chang’ombe, Dk. Kitila Mkumbo.
Mwenyekiti huyo alivitaja vyuo vitakavyoshiriki kuwa ni Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (UDSM), Taasisi ya Utawala wa Fedha (IFM), Chuo Kikuu cha
Ardhi (ARU), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha
Kampala (KIU), Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Teknolojia ya Madawa (IMTU),
Chuo cha Ustawi wa Jamii, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohane na Chuo Kikuu
cha Muhimbili.
No comments:
Post a Comment