RAIS Jakaya Kikwete amekiri kuwa Tanzania bado inakabiliwa na
changamoto ya uwezo katika sekta ya nishati ambayo ni muhimu katika
kuleta maendeleo ya nchi na wananchi wake kwa ujumla.
Kikwete amesema hayo wakati anachangia katika mjadala maalumu kuhusu
uhamasishaji wa sekta binafsi katika kuwekeza kwenye sekta ya nishati
barani Afrika ambao umeongozwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID)
na kuratibiwa na kiongozi wake, Rajiv Shah.
“Uwezo wa kuzalisha na kuusambaza bado ni changamoto kwetu, tunataka
kuacha kutegemea umeme we maji pekee na kuanza kuzalisha kwa njia
zingine mbadala, lakini bado uwezo wetu kama serikali ni mdogo na
tumeamua kuwashirikisha watu binafsi ili umeme huu uweze kuwafikia
wananchi walio wengi zaidi,” alisema.
Rais Kikwete yuko mjini Davos, Uswisi kuhudhuria kikao cha kila mwaka
cha uchumi ambapo viongozi mbalimbali wa nchi, wakurugenzi wa mashirika
na makampuni makubwa duniani huhudhuria kwa ajili ya kujadili
changamoto, matumaini na mapendekezo kadhaa kwa lengo la kukuza na
kuimarisha uchumi duniani.
Kikao chicho pia kimehudhuriwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza,
Tony Blair, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Haile Mariam Desalegne na Rais wa
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB), Donald Kaberuka.
Katika kikao kingine ambacho kimehusu kilimo na usalama wa chakula
barani Afrika, Rais Kikwete alisema Tanzania imetengeneza mkakati
maalumu kuhusu kilimo ambao unatekelezwa kama ulivyopangwa.
Alisema pia kuwa kumekuwa na upotoshwaji kuhusu uwekezaji mkubwa
katika kilimo ambao umetafsiriwa Kama uporaji wa ardhi ya wananchi.
“Tanzania tunayo ardhi, na ile tunayotoa kwa wakulima wakubwa ni ardhi
iliyotengwa na serikali kwa ajili ya wakulima wakubwa (land bank),”
alisema.
Rais Kikwete alitumia nafasi hiyo pia kukutana na kufanya mazungumzo
na viongozi kadhaa wa nchi na wa makampuni binafsi waliopo Davos kwa
ajili ya mkutano wa uchumi.
Pia alipata fursa ya kuzungumza katika chakula maalumu kilichoandaliwa
na Shirika la Roll Back Malaria ambapo washiriki walizungumzia suala la
diplomasia na afya.
Katika hilo, Rais Kikwete
alisema serikali pekee haziwezi kutatua changamoto za afya, hivyo zinahitajika pia juhudi za nchi rafiki na mashirika binafsi.
“Tunahitaji kuimarisha huu uhusiano na kuendelea kufanya kazi pamoja
kwani serikali zinahitaji sana wenza katika kutatua changamoto nyingi
zilizopo katika sekta ya afya kwani kunahitajika nguvu zaidi ya zile za
serikali,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment