NAIBU Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos
Makalla, amekerwa na kitendo cha uongozi wa timu ya Simba kupanga nyota
chipukizi katika mechi ya kirafiki dhidi ya Black Leopard ya Afrika
Kusini iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, juzi.
Katika mechi hiyo iliyoisha kwa Simba kufungwa bao 1-0, hakuna nyota
hata mmoja wa kikosi cha kwanza aliyepangwa, licha ya mashabiki kuwa na
shauku ya kukiona kikosi cha Simba kilichorejea hivi karibuni kutoka
kambini nchini Oman.
Waziri Makalla alisema, kitendo hicho hakipaswi kufumbiwa macho, kwani
kinawakatisha tamaa mashabiki, akiwemo yeye ambaye alikuwepo,
waliokwenda uwanjani kuwaona Simba, lakini wakaishia kuwaona ‘chekechea’
kwenye mechi hiyo.
Alisema jambo hilo lina athari kubwa katika mustakabali wa soka
nchini, kwani linawavunja moyo mashabiki, hivyo siku nyingine
kutojitokeza uwanjani kwa hofu ya kuingizwa mkenge.
“Kama mashabiki walielezwa ni mechi ya Simba na Black Leopard,
walipaswa kuiona Simba ikicheza, sio kikosi cha pili kama ilivyokuwa
jana,” alisema Makalla.
Alisema kitendo hicho hakipaswi kufumbiwa macho, kwani sio tu
hakiwatendei haki wapenzi na mashabiki, bali pia siku nyingine watasita
kujitokeza viwanjani kushuhudia mechi za kirafiki, kitu ambacho si
kizuri kwenye soka.
Mbali ya waziri kukerwa na kitendo hicho, hata mashabiki wa Simba na
Yanga waligubikwa na hasira mara baada ya kuona kikosi cha vijana cha
Simba kikitua dimbani kuwakabili Black Leopards, ikiwa ni nje ya
makubaliano ya mchezo huo.
Baada ya kikosi hicho kuingia uwanjani, mashabiki walianza kuwaponda
na kuwazomea viongozi wa Simba, wakidai ni wababaishaji na kwenda mbali
zaidi kwamba ni sawa na kamari ya mitaani, ambayo sawa na wizi wa wazi,
kwani walitarajia kuiona Simba ya Oman.
Shabiki Juma Saidi alisema, kitendo kilichofanywa na uongozi wa Simba
kimemsikitisha, kwani akiwa mpenzi wa timu hiyo, alikwenda uwanjani na
kulipa kiingilio kwa lengo la kuishuhudia Simba ikicheza baada ya
maandalizi ya Oman.
“Mimi ni shabiki mkubwa wa Simba, lakini kitendo cha viongozi wetu
kuchezesha kikosi cha watoto wakati sisi tulitegemea kuona kikosi cha
Oman tuone maandalizi ya huko, kama ni hivyo waendelee kuwachezesha hao
hata Ligi Kuu,” alisema shabiki huyo.
Mwingine ni Chalz Baba, Rais wa Bendi ya Mashujaa, aliyesema kuwa
amekerwa na kitendo hicho, kwani alikwenda kuwaona Simba waliotoka Oman
sio vijana.
Katika mechi hiyo, Simba iliwakilishwa na Abuu Hashim, William Weta,
Emiry Mgeta, Hassan Isihaka, Hassan Hatib/Haruna Shamte, Saidi Ndemla,
Ramadhan Singano, Ibrahim Ajid, Marid Kaheza, Rashid Ismail, Miraji
Kadenge.
No comments:
Post a Comment