Na Mwandishi wetu, Tabora
WAZIRI wa ujenzi, John Magufuli ametangaza kumsimamisha kazi
mkandarasi wa kampuni ya Progressive Constructions Ltd - Higleig Joint
Venture anayejenga barabara ya Songea – Namtumbo – Kilimansera hadi
Matemanga.
Magufuli alifikia uamuzi huo jana wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa
miradi minne mikubwa iliyozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete ambayo
inajengwa kwa kiwango cha lami mkoani Tabora.
Magufuli alisema kuwa Mkandarasi Progrissive ameshindwa kutekeleza
kazi kwa mujibu wa mkataba, hivyo amesimamishwa huku vifaa vyake
vikizuiliwa.
Aidha Rais Kikwete alizindua ujenzi wa miradi hiyo ikiwa ni pamoja na
barabara ya Nzega – Puge – Tabora yenye urefu wa kilometa 114.9
inayounganisha mji wa Nzega na makao makuu ya mkoa huo ambao
unaunganisha Tanzania na nchi jirani za Uganda, Rwanda na Burundi Rais
Kikwete alisema kuwa Serikali katika mkoa huo inatekeleza jumla ya
miradi mikubwa ya barabara minne yenye urefu wa kilometa 293.9 pamoja na
mradi wa ujenzi wa daraja la Mbutu.
Naye Mtendaji Mkuu wa Tanroads Injinia Patrick Mfugale, alisema mradi
huo unagharimu kiasi cha sh. bilioni 135 na unajengwa na Kampuni za
‘China Communications Construction Company Ltd (CCCC) kwa sehemu ya
Nzega-Puge yenye urefu wa km 58.8.
“Huku kampuni ya ‘Sinohydro Corporation Ltd’ inajenga sehemu ya Puge
– Tabora yenye urefu wa km 56.10 zote za kutoka nchini China
zinazosimamiwa na Kampuni ya ‘SMEC International (PTY) Ltd’ ya
Australia,” alisema.
Alisema mradi mwingine uliozinduliwa ni ujenzi wa sehemu ya barabara
inayotokea Itigi mkoani Singida kupitia Tabora hadi Urambo ambayo
inaenda hadi Kigoma.
“Pia barabara nyingine iliyozinduliwa ni kuanzia Nyahua kupitia Tabora
hadi Ndono yenye urefu wa kilometa 127 ambayo inajengwa na makandarasi
wawili kwa gharama ya Sh. bilioni 151,” alisema.
Alisema kuwa barabara hizo zitaondoa kilio cha wakazi wa eneo hilo cha
kukosa mawasiliano yenye uhakika kwa njia ya barabara za kuwaunganisha
na mikoa mingine jirani.
No comments:
Post a Comment