MWANDISHI na Mtangazaji wa Kituo cha Redio Kwizera, Wilayani
Kibondo, mkoani Kigoma, Issa Ngumba ameuawa kwa kunyongwa na watu
wasiojulikana.
Tukio hili la kusikitisha, limetokea juzi wilayani humo baada ya mwandishi huyo kupotea kwa siku tatu.
Habari kutoka wilayani Kibondo zinasema kuwa mwili wa marehemu ulikutwa porini jana ukikutwa na matundu ya risasi.
Taarifa zinasema kuwa marehemu ambaye alikwenda mapumziko nyumbani
kwao Muhange akitokea Kakonko, mwili wake uligundulika porini na
ulikutwa bastola yenye risasi tano na pembeni kulikuwa na simu mbili za
mkononi.
“Taarifa za daktari zinaonesha kuwa marehemu alinyongwa shingo na
kupigwa risasi,” alisema mtoa habari wetu kutoka wilayani Kibondo.
Uchunguzi umebaini kuwa watu hao hawakuwa na dhamira ya kumuibia kwani
hawakuchukua kitu chochote kwani hata simu zake mbili za mkononi
zilikutwa zimetelekezwa kando ya mwili wake.
Hata hivyo taarifa zaidi zinasema kuwa mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa umenyofolewa baadhi ya viungo, zikiwemo sehemu nyeti.
“Hawa wauaji walikuwa na lengo la kutoa uhai maana hawakumuibia fedha
wala simu kwa kuwa marehemu alikutwa na noti ya shilingi 10,000
mfukoni,” alisema.
Taarifa za kipolisi kutoka mkoani Kigoma zinasema kuwa kazi ya
uchunguzi wa tukio hili imeanza wakati taratibu za mazishi zinafanyika.
No comments:
Post a Comment