Habari na Farida Ramadhani
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, ametaka madaraka ya rais yadhibitiwe ili kumwezesha kufamya kazi kwa ufanisi zaidi.
Alisema si lazima kila kitu aamue rais wakati ana wasaidizi wake ambao wanaweza kurahisisha utendaji wake.
“Sote tunajua rais ana majukumu mengi lakini si lazima yote ayafanye
yeye, anaweza hata kusaidiwa na Makamu wa Rais kwenye vitu kama uteuzi
na kushughulikia mambo ya kinidhamu,” alisema.
Akizungumza na waaandashi wa habari jijini Dar es Salaam jana baada ya
kuwasilisha maoni ya mabadiliko ya Katiba, Pinda pia alipendekeza
mawaziri wasitokane na wabunge ili kuwawezesha kutekeleza vizuri
majukumu yao.
Kwa mujibu wa Pinda, mawaziri wengi wamekuwa wakibanwa na shughuli za
kiserikali na kushindwa kutekeleza shughuli za Bunge ambazo ndizo
zimewafanya wafike bungeni na kuteuliwa kuwa mawaziri.
Katika suala la Muungano, Pinda alipendekeza kuwe na serikali mbili
kama ilivyo sasa lakini kuwe na tume maaalumu itakayoshughulikia
matatizo ya Muungano.
“Najua serikali mbili zina kero nyingi lakini dawa si kuziondoa ila
tuunde tume ya kushughulikia kero hizo, nadhani kila kitu kitakwenda
sawa, sioni sababu ya watu kung’ang’ania kutengana kwa sababu ya mafuta
au gesi, kama mafuta yapo Zanzibar itarahisisha badala ya kununua
Uarabuni tuyapate karibu,” alisema.
Waziri mkuu huyo pia alipendekeza kazi za mihimili mitatu (Bunge,
Mahakama na Serikali), ziainishwe katika katiba mpya ili kuzuia
muingiliano wa kazi, kwani mihimili hiyo imekuwa ikitegemeana katika
kutimiza kazi zake.
Waziri mkuu huyo pia alipendekeza katiba mpya iwe na kipengele
kinachoruhusu Serikali za Mitaa kuwa huru kufanya kazi zao na ioneshe
wazi majukumu pamoja na mgawanyo kati ya Serikali Kuu na Serikali za
Mitaa.
Alisema kwa muda mrefu sasa, Seriakli za Mitaa zimekuwa zikitegemea
kila kitu kutoka Serikali Kuu lakini haoni sababu ya kupewa jina la
serikali wakati haziko huru.
Hata hivyo Pinda aliupongeza mfumo mzima wa mchakato wa kukusanya
maoni ya katiba mpya kwa kuwa umeandaliwa na kusimamiwa na Watanzania.
Awali, Mwanasheria Mkuu mstaafu, Jaji Damian Lubuva, alifikisha maoni
yake katika tume hiyo na kupendekeza katiba ijayo iwe na kipengele
kinachoruhusu kuwa na jopo maalumu la kupendekeza majina ya majaji na
rais apewe majina hayo kwa ajili ya uteuzi, badala ya uteuzi huo
kufanywa na kuthibitishwa na rais mwenyewe.
Lubuva alipendekeza muda wa majaji kustaafu uongezwe hadi kufikia
miaka 70 kwa majaji wa Mahakama Kuu na miaka 72 kwa majaji wa Mahakama
ya Rufaa.
Mwanasheria huyo alipendekeza katiba mpya ianzishe mahakama ambayo
itaitwa ‘Supreme Court’, itakayowezesha wananchi kutoa malalamiko yao
iwapo hawataridhika na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa.
Aliongezea kuwa katiba iainishe Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kabla ya
kutaja majukumu ya Mwanasheria Mkuu pamoja na kufanya marekebisho ya
kuainisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kabla ya kushughulikia
uteuzi wa shughuli zake ili kuimarisha uhuru katika utendaji kazi wake.
“Itamkwe bayana katika utendaji kazi kuwa DPP anaweza kuondoshwa
madarakani tu kwa sababu zitakazoainishwa kama vile kutomudu kufanya
kazi kwa sababu ya ugonjwa au kushindwa kufanya hivyo,” alisema.
No comments:
Post a Comment