MKAKATI wa Spika wa Bunge, Anna Makinda, kutaka kuitetea
serikali hata pale inapofanya madudu ya wazi, umeelezwa kuwa chanzo cha
kuvurunda kiutendaji kwa kiongozi huo wa muhimili wa dola.
Kutokana na udhaifu huo, Makinda amejikuta akibebeshwa lawama kutoka
kwa wananchi, wafuasi wa vyama vya upinzani na kibaya zaidi hata baadhi
ya viongozi wa juu na wabunge wa chama chake ambao baadhi wanadaiwa
kusuka mkakati kutaka kumg’oa.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili mjini Dodoma hivi karibuni,
mkakati huo unaongozwa na baadhi ya wabunge wa CCM wanawake ambao tangu
awali hawakuunga mkono namna alivyoingia Bungeni kushika wadhifa huo.
Wapinzani hao wa Spika hasa wale wa kutoka ndani ya CCM, wameingiwa
wasiwasi kwamba mwenendo wake wa kutaka kuibeba serikali, unawapa
umaarufu wabunge wa upinzani na hivyo kuweka mazingira magumu ya CCM
kushinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Katika mkutano wa kumi wa Bunge uliopita, Spika pamoja na Naibu wake,
Job Ndugai, walionyesha udhaifu wa waziwazi wa kuibeba serikali pale
walipoamua kupindisha kanuni kuibeba serikali.
Kiti cha Spika kilizima hoja mbili binafsi za Mbunge wa Ubungo, John
Mnyika (CHADEMA), aliyekuwa na hoja ya kuboresha huduma ya maji katika
jiji la Dar es Salaam na James Mbatia (NCCR-Mageuzi), aliyezimwa na
hoja ya udhaifu wa mfumo wa elimu nchini.
Matumizi mabaya ya kanuni zilizotumika kuzima hoja hizo, uliibua
vurugu na mzozo mkubwa na wa kwanza katika historia ya Bunge la Tanzania
na kusababisha kuzima hoja nyingine binafsi mbili.
Spika Makinda amejikuta katika lawama kubwa zaidi pale kiti chake
kiliporuhusu kupitisha mapendekezo ya serikali kufanya mabadiliko katika
Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma ya mwaka 2008 na kuvunja kamati za
Bunge.
Katika mapendekezo hayo, serikali imeongeza vifungu vinavyopunguza
nguvu ya Bunge katika kushughulikia taarifa ya Ofisi ya Mkaguzi na
Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, umebaini kuwa muswada huo wa sheria ambao ulipita kwa
mbinde kutokana na upinzani wa wabunge wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), ulikuwa na nia ya kuwadhibiti wabunge wa kambi ya
upinzani ili kuinusuru serikali.
Kwa mujibu wa ibara ya 143 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, (CAG)
anawajibika kuwasilisha taarifa yake kwa Rais ambaye baada ya kuipitia,
atawasilisha taarifa hiyo kwenye kikao cha Bunge kilicho karibu kabla
ya kupita siku saba tangu kikao hicho cha Bunge kuanza.
Chini ya mabadiliko hayo sasa, ripoti za CAG baada ya kutoka kwa Rais,
itawasilishwa na kujadiliwa katika kamati tatu zinazosimamia hesabu za
serikali kwa ajili ya kufanya uchambuzi, kisha kuwasilisha Bungeni
katika muda zitakaopangiwa.
Wachambuzi wa duru za siasa wanasema kuwa kwa mabadiliko hayo, Bunge
halitakuwa tena na uwezo wa kuwawajibisha watendaji wa serikali ambao
watabainika kuhusika na upotevu wa fedha au kufuja fedha za umma, hivyo
kupunguza makali ya mijadala ya wabunge wa upinzani Bungeni.
“Hatua hiyo ni sawa na kulifunga mikono Bunge kutekeleza wajibu wake
kuhusu ripoti ya CAG kwani halitaweza kujadli chochote kabla ya serikali
kuipitia na kuipatia majibu yake,” alisema mtoa habari wetu.
Hata hivyo kamati za Bunge ambazo taarifa za CAG zinapaswa
kuwasilishwa ni zile za hesabu za mashirika ya umma (POAC), iliyokuwa
ikiongozwa na Zitto Kabwe ambayo kwa sasa imefutwa.
Kamati nyingine ni ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC),
inayoongozwa na Mbunge wa Augustine Mrema (TLP) na Kamati ya Hesabu za
Serikali Kuu (PAC), iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa Bariadi Mashariki,
John Cheyo (UDP).
Hata hivyo wakati marekebisho hayo ya sheria yanafanyika na
kupendekeza taarifa hizo ziwasilishwe kwenye kamati hizo, Spika Makinda
kwa mamlaka aliyopewa amezifuta baadhi na kuziunganisha zingine kuwa
moja.
Habari kutoka ndani ya ofisi ya Mwanasheria wa Serikali (AG), zilisema
kuwa lengo la mabadiliko hayo ni kuikoa serikali na hoja za wabunge wa
upinzani ambao mwaka jana nusura waiangushe serikali.
“Hatua hiyo itaiokoa serikali kwani utaratibu mzima wa kushughulikia
taarifa hizo umebadilika na vimeongezwa vipengele vinavyoliwajibisha
Bunge kwa serikali. Vipengele hivi vinazitaka kamati za Bunge
zinapofanya uchambuzi wa ripoti ya CAG, kupeleka maazimio yake kwa
serikali ili yatafutiwe majibu badala ya utaratibu wa sasa wa kupeleka
hesabu zake moja kwa moja Bungeni,” alisema mtoa habari wetu kutoka
ofisi ya CAG.
Kwa mujibu wa habari hizo, serikali imeleta mabadiliko hayo ambapo
chini ya utaratibu huo, itakuwa na majibu ya hoja za wabunge tofauti na
utaratibu wa zamani ambapo haikuwa rahisi kwa serikali kuwa na majibu
sahihi.
Mwaka jana, Rais Kikwete alilazimika kufanya mabadiliko katika Baraza
la Mawaziri na kuwaondoa mawaziri Sitta na Manaibu Waziri wawili, yakiwa
ni matokeo ya mjadala wa ripoti ya CAG ambayo ilibainisha kuwapo kwa
madudu mengi.
No comments:
Post a Comment