Padre Evarist Mushi alie uwawa asubuhi ya jana |
MATUKIO yenye taswira ya udini yameendelea kujirudia visiwani
Zanzibar ambapo watu wasiofahamika, wamemuua kwa kumpiga risasi Padri wa
Kanisa Katoliki Parokia ya Minara Miwili, Evarist Mushi, jana asubuhi
wakati akiegesha gari lake kanisani hapo.
Hili ni tukio la tatu kutokea visiwani humo ndani ya muda mfupi kwa
viongozi wa dini kushambuliwa na kuumizwa, kwani Novemba 5 mwaka jana,
Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga alimwagiwa
tindikali na mtu asiyefahamika iliyomwathiri sehemu kubwa ya mwili wake.
Desemba 26 mwaka jana, watu wasiojulikana walimpiga risasi Padri
Ambros Mkenda wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mpendae mjini Zanzibar na
kumjeruhi.
Waumini wa kanisa hilo walioshuhudia tukio, walisema kuwa kabla ya
Padri Mushi kufika eneo la kanisa, walionekana watu wawili ambao
walikuwa na pikipiki wakiwa wamesimama kando ya barabara.
Kwamba alipoingia padri huyo eneo la kanisa kwa ajili ya kuongoza
ibada, watu hao walimfuata na kumshambulia wakati akiegesha gari lake,
na kisha kukimbia kusikojulikana.
Waumini hao ambao walikusanyika katika Hospitali ya Mnazi Mmoja,
ulipohifadhiwa mwili wa marehemu, waliiomba serikali ichukue hatua kwa
wahalifu hao, wakidai matukio hayo yamekuwa yakiwalenga Wakristo.
Akithibitisha tukio hilo, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Musa Ali Musa
alisema kuwa wanaendelea kuwasaka watuhumiwa hao kuwaomba wananchi kutoa
msaada wa taarifa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdallah Mwinyi aliiomba
serikali kuchukua hatua kwani wahalifu hao wanataka kuleta mfarakano
kati ya Wakristo na Waislamu.
Kanisa laanda tamko
Askofu wa Jimbo la Zanzibar, Augustino Shayo alifika hospitalini hapo
na kujadiliana na baadhi ya viongozi, na baadae mmoja wa viongozi
waliokuwa na waumini hao kuwatangazia kurudi kanisani kuendelea na
ibada.
Hata hivyo, waumini hao walipinga jambo hilo na kusema kuwa
wataendelea kuwapo hapo hadi haki yao ipatikane, huku wengine wakitaka
kuandamana ili kuonesha machungu yao.
“Leo tunaandamana tumechoka, tukio la kwanza tumevumilia na hili pia,
hapa haki yetu ipo wapi? Tunamtaka Waziri wa Ulinzi kutoa tamko tukiwa
hapa hapa," alisema mmoja wa waumini hao.
Kiongozi huyo alirudia tena kuwasihi waumini hao kuwa na moyo wa
uvumilivu kama mafundisho ya dini na imani, na kuwaomba waelekee nyumba
ya ibada kuendelea na misa ama kurudi majumbani, lakini hawakutii agizo
hilo.
Akitoa msimamo wa kanisa majira ya saa nane mchana, msaidizi wa
askofu, Padri John Mfoi aliwataka waumini kurudi nyumbani, na kwamba
viongozi wakuu watatoa tamko rasmi hapo baadaye.
"Tayari uchunguzi umeshafanyika na kilichobaki sasa wanamshona na
tunasubiri kuoshwa na kisha kuhifadhiwa rasmi. Viongozi wetu wanatarajia
kukutana mapema jioni kupanga taratibu zote husika,” aliongeza Padri
Mfoi.
Polisi wajipanga
Kufuatia mauaji hayo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said
Mwema, alisema kuwa wanawashikilia watu watatu kuhusiana na tukio hilo.
Akizungumza na waandishi Dar es Salaam jana, Mwema alisema kuwa mara
baada ya kupokea taarifa hizo tayari timu ya watu watatu imeenda kwa
ajili ya kuanza kazi za kiuchunguzi.
“Taarifa hizo ni za kusikitisha sana na tayari nimetuma timu ya
wataalamu waliobobea kwenye masuala ya upelelezi kwenda kufuatilia suala
hilo, na tutawakamata tu kwa kuwa tunaweza kupambana na majambazi
hatuwezi kuwashindwa wahalifu,” alisema.
Aliitaja timu ya upelelezi iliyokwenda Zanzibar kuwa ni Naibu Kamishna
Samson Kasala ambaye atakuwa mpelelezi, Naibu Kamishna Peter Kivuyo kwa
ajili ya ukusanyaji taarifa mbalimbali na Simon Siro kwa ajili ya
operesheni.
Mwema alizitaja namba za mawasiliano kwa ajili ya kufanikisha
upelelezi huo kuwa ni 0754 785557 na 0782 417247, na pia alishauri
kutumika kwa namba za makamanda wa polisi wa mikoa, huku akiwataka
wananchi kutoa taarifa zozote kuhusiana na tukio hilo kupitia namba
hizo.
Alipoulizwa kama mauaji hayo yanahusiana na mtandao wa kundi la
Al-Qaeda, Mwema alisema kuwa wamekuwa wakilifuatilia ili kujua lipo
kundi hilo.
Kuhusu lawama za jeshi hilo kuchelewa kuchukua hatua nzito kama hii ya
kuunda kundi la wapelezi walivyofanya sasa, alisema kuwa wamefanya
hivyo mara kadhaa isipokuwa taarifa hazitolewi kwa uwazi kwa waandishi.
Alipoulizwa kama suala hilo linahusiana na masuala ya dini au siasa, Mwema alidai kuwa kuna mwelekeo huo.
Mbowe aivaa serikali
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimelaani matukio ya
vurugu na
mauaji yenye misingi ya tofauti za kidini, huku kikidai ni matunda ya
mbegu ya udini na ukabila uliopandikizwa na Serikali ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kwa nia ya
kuvidhoofisha vyama vya upinzani.
Akifungua kikao cha viongozi wa chama hicho Kanda ya Kaskazini jijini
Arusha jana, Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe aliitaka CCM
na serikali yake kuhakikisha nchi inakuwa salama.
Alisema CCM kwa kudhani inavikomesha vyama vya upinzani, iliasisi,
kueneza na kushabikia sera na chochoko za ubaguzi wa kidini kwa
kuwadanganya wananchi kuwa, baadhi ya vyama ni vya kidini na kikabila,
matokeo yake sasa udini umeanza kuwa kansa inayoitafuna taifa.
“CCM walidhani chokochoko za udini na ukabila zitaviangamiza vyama vya
upinzani na kukisaidia kuendelea kusalia madarakani. Hawakujua
wanapandikiza mbegu mbaya miongoni mwa Watanzania waliozoea kuishi kwa
amani na umoja bila kujali tofauti zao za kidini na kikabila,” alisema.
Mbowe alisema kuwa CCM wamelikoroga, sasa lazima walinywe kwa kuhakikisha taifa linakuwa moja na lenye amani.
Alisema siyo sahihi viongozi wa dini, wawe masheikh, wachungaji,
mapadri au mtu awaye yote, kushambuliwa, kumwagiwa tindikali wala kuuawa
katika matukio yenye hisia na sura za kidini.
Mbowe alisema ni jukumu na wajibu wa serikali kuwahakikishia raia wake usalama wa maisha na mali zao.
Alisema chama chake kinaamini katika misingi ya taifa lenye haki,
amani, umoja na mshikamano kwa watu wote bila kujali tofauti za kidini
na kikabila.
Mbowe alisema misingi ya watu makabila yote hapa nchini wa imani
tofauti za
kidini, ya kuishi kwa kuheshimiana na kushirikiana, lazima ilindwe na
kuendelezwa kwa kila mtu kutekeleza jukumu lake la kuenzi tunu hiyo
iliyoasisiwa na kupiganiwa na waasisi wa taifa.
Katika vipindi tofauti, viongozi wa CCM na serikali yake walikaririwa
wakitangaza kuwa Chama cha Wananchi (CUF) na CHADEMA vina misingi ya
kidini na kikabila kama moja ya mbinu za propaganda.
JK aomboleza
Rais Jakaya Kikwete ameeleza kupokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya kuuawa kwa Padri Mushi mjini Zanzibar.
Katika taarifa yake kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais
Kikwete aliwapa pole na rambirambi za dhati ya moyo wake Baba Askofu
Shayo wa Jimbo Katoliki la Zanzibar na waumini wote wa Parokia ya Minara
Miwili kwa msiba huo mkubwa uliowakuta.
“Napenda kuwahakikishia kuwa tupo pamoja katika kuomboleza kifo cha
mpendwa marehemu Padri Mushi na msiba huu ni wa kwetu sote,” alisema.
Rais Kikwete alisema kuwa ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kukusanya
nguvu zake zote na maarifa yake yote kuhakikisha kuwa uchunguzi wa kina
na wa haraka unafanyika ili kubaini mhusika ama wahusika, na kuwakamata
ili kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.
Alisema kuwa anataka ukweli wake ujulikane ili kama kuna jambo lolote zaidi liweze kushughulikiwa na kukata mzizi wa fitina.
Waziri Nchimbi awasili
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi aliwasili
visiwani hapa na kutembelea eneo la tukio alipouawa padre huyo kisha
alifanya mazungumzo na waandishi wa habari.
Alisena tukio hilo ni la kigaidi, hivyo serikali haitalivumilia kamwe, na kuahidi kulishughulikia ili kuwabaini wahusika.
Nchimbi aliwataka waumini hao kuwa na utulivu kwa kipindi hiki, huku
uchunguzi wa kina ukiendelea na kuvitaka vyombo vya ulinzi vya ndani na
nje kushughulikia suala hilo.
No comments:
Post a Comment