SAKATA la gesi limetua rasmi bungeni baada ya Kiongozi wa Kambi
ya Upinzani, Freeman Mbowe kuitaka Serikali iweke hadharani mikataba ya
utengenezaji wa bomba la kusafirishia gesi hiyo kutoka Mtwara kwenda Dar
es Salaam ili kuondoa usiri uliogubika mradi huo.
Mbowe alitoa wito huo jana alipokuwa akimuuliza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda maswali bungeni katika kipindi cha Maswali na Majibu kwa Waziri Mkuu.
Mbowe alitoa wito huo jana alipokuwa akimuuliza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda maswali bungeni katika kipindi cha Maswali na Majibu kwa Waziri Mkuu.
Kiongozi huyo wa upinzani alimtaka Waziri Mkuu kueleza ni kwa nini Serikali isiweke wazi mikataba yote ya gesi ili kuondoa hofu iliyojengeka kwa wananchi kwamba kumekuwa na hali ya ufisadi.
Akijibu swali hilo, Pinda aliwataka wabunge kutumia utaratibu mzuri wa kupata mikataba hiyo akisema haiwezekani ikawekwa hadharani.
Mbali na jibu hilo, Pinda alivitupia lawama vyama vya siasa akisema vimechangia kwa kiasi kikubwa mgogoro wa gesi mkoani Mtwara.
Licha ya juzi kueleza kuwa kulikuwa na
mgogoro wa viongozi ndani ya mkoa huo pamoja na CCM, jana alikwepa swali
la kutaka wahusika wawajibike na badala yake akasema suala hilo liko
juu yake.
Alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali lingine la Mbowe ambaye alimtaka Pinda kutoa kauli juu ya nani aliyesababisha mgogoro wa Mtwara uliosababisha maafa.
Hata hivyo, alitangaza neema kwa waathirika kwamba Serikali inaangalia namna ya kuwapunguzia gharama wale wote waliopatwa na matatizo hayo ikiwamo kuwalipa fidia.
“Vyama vya siasa vimechangia kwa kiasi kikubwa katika kupotosha jambo hilo, ushindani wa chaguzi zinazokuja umejitokeza pia,” alijibu Pinda.
Kiongozi huyo alisema wanaofanya uchochezi huo wanafanya bila ya kujua kwamba unaweza kuwakumba watu wote wakiwamo hao wanaofanya hivyo.
“Tutalaumiana wengi lakini ni vyema kuweka mambo hadharani na kwamba ni hatari kufanya mambo kama hayo kwani amani ya nchi ni lulu ambayo ikipotea inaweza kuwa tabu kuipata.”
Alipinga hoja ya Mbowe kuwa Serikali inatekeleza majukumu yake baada ya shinikizo na maandamano ya wanasiasa.
Alilieleza Bunge kuwa wananchi wa Mtwara wanaweza
kupoteza fursa nyingi kutokana na wawekezaji kuanza kuondoka wakikwepa
vurugu na kukimbilia Msumbiji ambako kuna dalili za gesi pia.
Kamati ya Makinda yayeyuka
Jana, Spika wa Bunge Anne Makinda aliliambia Bunge kuwa Kamati aliyotarajia kuiunda haitakuwapo kutokana na ukweli waliokuwa wakiutaka kutoka Mtwara kuelezwa na Waziri Mkuu.
Akiahirisha Bunge mchana wa Januari 29, mwaka huu, Makinda alitangaza kuwa angeunda kamati ya Bunge kwenda Mtwara kuangalia mgogoro huo.
“Kutokana na ukweli uliotolewa na Waziri Mkuu leo bungeni, naomba nimshukuru sana kwa dhati kwa kulishughulikia tatizo la Mtwara, lakini nieleze kuwa nilikusudia kuunda tume kwa ajili ya kwenda kutazama suala hilo, lakini tayari tumepata ukweli hivyo naona haina haja ya kuunda tume hiyo,” alitangaza Makinda.
Moto bungeni
Hoja binafsi ya Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia inayokosoa mfumo wa elimu Tanzania kwa shule za msingi na sekondari kuwa ni dhaifu na hauleti matumaini kwa wanafunzi, ilizua mjadala mzito bungeni jana baada ya Serikali kukataa pendekezo lake la kuunda kamati maalumu ya kutafuta chanzo cha tatizo hilo.
“Kutokana na hayo, ninaliomba Bunge lako tukufu kuunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza kina cha udhaifu huo wa kimfumo katika sekta ya elimu hapa nchini na kupendekeza hatua za kuchukua ili taifa liondokane na aibu ya udhaifu huo,” alisema Mbatia.
Baada ya hoja hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alipangua hoja moja baada ya nyingine na kuliomba Bunge lisikubali kuundwa kwa kamati teule, bali liiagize Serikali kushughulikia suala hilo.
Baada ya Dk Kawambwa kutoa hoja hiyo, Mbatia alisimama na kuikataa akisema kile alichokiainisha juu ya udhaifu hakifanani na kutaka kuundwa kamati kupitia kila hatua yenye udhaifu.
Baada ya Mbatia kusema hayo, ulizuka ubishi baada ya Spika Makinda kutaka kujadiliwa kwa mabadiliko ambayo Serikali inataka au hoja ya Mbatia iendelee.
Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisema kuna kila sababu ya kuunda kamati lakini iwe teule ya Bunge.
“Tunatakiwa tujadili kwanza hoja iliyoko mezani na si kujadili mabadiliko ya hoja Mheshimiwa Spika, hoja aliyotoa Mbatia isibadilishwe kwa kuwa ni kinyume na kanuni za Bunge lako tukufu,” alisema Lissu.
Baadaye walisimama wabunge zaidi ya watatu wakitaka kuchangia lakini Spika Makinda alitoa nafasi kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi ambaye alisema: “Tukiunda tume itachukua muda... Hoja iliyotolewa na Mbatia ni ya msingi, sasa kamati za Spika zishirikiane na Wizara ya Elimu kufanya kazi hiyo.”
Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekiah Wenje alisema haiwezekani Bunge likakubali Serikali ijichunguze yenyewe kwa kuwa ni kitu ambacho hakikubaliki na ni kinyume cha kanuni za Bunge.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM) alisema kuna matatizo katika sera, mitalaa na muhtasari na kusema sasa ni kazi ya Bunge kupata tume stahiki.
No comments:
Post a Comment