VITENDO vya uchomaji makanisa moto vimeendelea kutikisa mji wa
Zanzibar baada ya Kanisa la The Pool of Siloam, kuchomwa moto na watu
wasiojulikana.
Tukio hilo ambalo limetokea siku chache baada ya Padri wa Kanisa
Katoliki, Evarist Mushi, kuuawa kwa kupigwa risasi, limetokea jana
katika eneo la Kianga, mkoa wa Mjini Magharibi, kisiwani Unguja, jana.
Hali hiyo imezidisha hofu kwa viongozi wa dini na waumini wao, huku
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ikiimarisha ulinzi katika makanisa
yote mjini hapa.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa siku kadhaa sasa, umebaini
kuwapo kwa baadhi ya viongozi wa SMZ, wanaotajwa kufadhili vikundi vya
kigaidi kwa lengo la kufanikisha nia zao.
Duru za uchunguzi kutoka visiwani humo, zililiambia gazeti hili kuwa
baadhi ya wanaotajwa kuhusika wamo wanafanyakazi serikalini katika
nafasi za juu na wengine wamestaafu.
“Kwa nini hamjiulizi tangu matukio hayo yatokee hivi karibuni kuanzia
kwa sheikh aliyemwagiwa tindikali, kupigwa risasi kwa padri mwingine na
hatimaye kuuawa kwa Padri Mushi? Kweli serikali haiwajui?” alihoji
kiongozi mmoja wa SMZ ambaye anaeleza kukerwa na hali hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio la kuchomwa moto kwa
kanisa hilo la walokole jana, Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai
Zanzibar (DCI), Yussuf Ilembo, alisema kanisa hilo lilichomwa moto
majira saa 9:00 usiku wa kuamkia jana na kusababisha uharibifu mkubwa wa
mali za kanisa hilo.
Kamishina msadizi huyo wa polisi, alisema mlinzi wa kanisa, Mussa
Jackison, alivamiwa na watu watatu na kuanza kushambuliwa kwa mawe
lakini hakujeruhiwa kabla ya kutimua mbio.
Alisema baada ya mlinzi kufanikiwa kukimbia walikusanya mali za kanisa vikiwemo viti na mali zingine, kisha kuvichoma moto.
Hata hivyo alisema kwamba uchunguzi kuhusiana na tukio hilo umeanza lakini hakuna watu waliokamatwa hadi sasa.
“Kanisa limechomwa moto majira ya saa 9:00 usiku baada ya watu watatu
kumvamia mlinzi na kuanza kumrushia mawe,” alisema DCI Ilembo.
Akizungumza Mchungaji wa Kanisa hilo,
Penuel Wisdom, alisema alipokea taarifa za kanisa lake kuchomwa moto kwa
mshtuki mkubwa kutokana na ukweli kwamba hilo ni tukio la pili kwa
kanisa lake kuhujumiwa.
Alisema mwaka 2011, watu wasiopungua 80 walivamia kanisa lake na
kulibomoa kwa kutumia vifaa vizito, zikiwemo sululu na nyundo za
kuvunjia mawe.
Alisema katika tukio hilo, watu kadhaa walikamatwa na kukiri lakini hakuna hata mmoja aliyefikishwa katika vyombo vya sheria.
“Ombi letu kwa serikali ni kuimarisha ulinzi; tunaona usalama wa
viongozi na waumini unatoweka kwa kasi Zanzibar,” alisema mchungaji
huyo.
Alisema kwamba tangu kujengwa kwa kanisa hilo viongozi, waumini na
wananchi wa Kianga wamekuwa na ushirikiano mkubwa na kusaidiana mambo ya
msingi ya huduma za jamii kama kisima cha kanisa kutumiwa na majirani
pamoja na uongozi wa kanisa kuazima huduma za umeme kutoka nyumba za
jirani.
Hata hivyo alisema kwamba baada ya mradi wa ujenzi wa kanisa kuanza
katika eneo hilo viongozi wa msikiti wa Kianga waliwahi kuhoji uhalali
wa kujengwa kwa kanisa mahali hapo.
Alisema vyombo vya dola vinapaswa kufanya uchunguzi wa kina na wa
haraka kuwasaka watu wanaofanya vitendo hivyo kwa sababu wanatishia
amani na umoja wa kitaifa kwa wananchi wa Tanzania.
Akizungumza kwa njia ya simu Sheha wa Kianga, Taufiki Ramadhan,
alisema amepokea taarifa za kuchomwa moto kanisa hilo kwa masikitiko
makubwa kwani kitendo hicho kinakwenda kinyume na misingi ya haki za
binadamu.
Alisema makanisa Zanzibar yamekuwepo kwa miongo mingi na waumini wa
Kislamu na Wakiristo wamekuwa wakiishi pamoja bila ugomvi licha ya
kutofautiana imani zao za dini na kushirikiana shughuli za kijamii kama
kawaida.
Alisema hata utawala wa Kisultani ulikuwa ukiheshimu uhuru wa watu
kuabudu ndiyo maana Wakiristo walipewa maeneo ya ardhi kujenga makanisa
katikati ya mji mkongwe wa Zanzibar na utawala wa Sultan kabla ya
Mapinduzi ya mwaka 1964.
“Baada tu ya kupokea taarifa za kanisa kuchomwa moto niliwasiliana na
Mkuu wa Wilaya ya Magharibi na Viongozi wa Jeshi la Polisi nashukuru
walifika katika tukio na kuanza kufanya kazi ya uchunguzi,” alisema
Sheha Ramadhan.
Naye mlinzi, Mussa Jackson, alisema baada ya kuwaona watu wakinyatia
alijaribu kujitokeza ghafla aliona mvua ya mawe ikimwelemea na kuamua
kukimbilia ndani ya kanisa kabla ya kutokea dirishani.
“Hali ilikuwa mbaya, walianza kukusanya kila kitu na baadaye kuwasha moto,” alisema Jackson.
Alisema kwamba tukio hilo linamkumbusha mwaka 2011 baada ya watu
waliokuwa wakipinga kujengwa kwa kanisa hilo walipovamia na kulibomoa
wakiwa na silaha za jadi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Kusini Unguja Zanzibar, ACP Augustine Olomi,
alisema jana kuwa tukio hilo limetokea majira ya saa 9.30 usiku.
Amesema moto huo ulizuka baada ya kikundi cha watu watatu kuonekana
wakipita njia karibu na kanisa hilo na baada ya muda mlinzi wa kanisa
hilo alisikia kanisa likishambuliwa kwa mawe juu ya paa.
Amesema baada ya mlinzi huyo kubaini kuwepo kwa hatari, alilazimika
kukimbia kwenda kujificha lakini huku akiangalia kwa mbali
kinachoendelea.
Kamanda Olomi amesema moto huo ungeweza kusababisha athari kubwa kama usingedhibitiwa mapema.
Hata hivyo amesema uimara wa dari lililotengenezwa kwa Gibsam
umesaidia kuuzuia moto huo kuunguza paa na kuliteketeza kabisa kanisa
hilo.
Kamanda huyo alisema wameimarisha ulinzi katika makanisa yote, huku wakiendelea na uchunguzi wa matukio hayo.
Mkasa wa kanisa kuchomwa moto umeongeza idadi na kufikia makanisa 26 na baa 12 kwa muda wa miaka 10 visiwani humo.
Hata hivyo hakuna mtu hata mmoja aliyewahi kukamatwa kuhusiana na matukio hayo na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Matukio hayo yalifuatiwa na Katibu wa Mufti Zanzibar Shekh Fadhili
Suleiman Soraga kumwagiwa tindikali Novemba 6 na Padri wa Kanisa
Katoliki Ambrose Mkenda kupigwa risasi na kutibiwa Mhimbili Desemba 25
mwaka jana kabla ya kuuawa kwa kupigwa risasi Padri wa Evaristus Mushi
Jumapili iliyopita Zanzibar.
Padri Mushi anazikwa leo katika makaburi ya mapadiri huko Kitope Mkoa
wa Kaskazini Unguja, ambapo misa ya kuanga mwili wa marehemu itafanyika
katika Kanisa la St. Joseph Minara miwili katikati ya mji mkongwe wa
Zanzibar.
Chanzo Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment