Waumini wamzomea mbele ya Rais Shein
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud,
amechafua hali ya hewa wakati wa mazishi ya Padri Evaristus Mushi,
aliyeuawa kwa kupigwa risasi Visiwani Zanzibar.
Hali hiyo iliyosababisha waziri huyo azomewe, ilitokea jana kwenye
mazishi ya padri huyo, yaliyofanyika katika makaburi ya watawa, yaliyopo
eneo la Kitope, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Mbele ya Rais wa SMZ, Ali Mohamed Shein, Waziri huyo aliwachefua
maelfu ya Wakristo waliofurika kwenye mazishi hayo wakati akitoa salamu
za pole kutoka kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Katika salamu hizo, waziri huyo alianza vizuri kwa kutoa pole na
kwamba serikali imeguswa na kifo hicho na maumivu waliyonayo waumini
ndiyo iliyonayo pia serikali.
Lakini wakati akiendelea kutoa salamu hizo, alichafua hali ya hewa kwa
kusema kifo cha Padri Mushi kimetokana na mapenzi ya Mwenyezi Mungu.
“Ndugu zangu poleni kwa msiba huu, serikali imeguswa sana na kifo
hicho kama ndugu na waumini mlivyoguswa. Hata hivyo hii ni mipango na
mapenzi ya Mwenyezi Mungu…”
Kauli hiyo ilisababisha umati wa watu waliofurika katika makaburi hayo
kupaza sauti kwa kuzomea na kuikejeli Serikali ya SMZ kwamba kifo hicho
hakikutokana na mapenzi ya Mungu.
Katika zogo hilo, wapo waliopaza sauti kwa kusema kifo hicho
hakikutokana na mapenzi ya Mungu, kwani hakufa kwa ajali ya maji, ajali
ya gari wala kugongwa na gari.
“Hatutaki kusikia hilo, Padri Mushi hakufa kwa mapenzi ya Mungu.
Hatutaki kusikia… huo…” zilisikika sauti za baadhi ya watu waliohudhuria
mazishi hayo.
Wakati zogo hilo linaendelea, Waziri Aboud alishindwa kuendelea kutoa
salamu hizo, hali iliyosababisha Askofu wa Jimbo la Zanzibar, Dk.
Augustino Shao kuingilia kati.
Shao aliungana na waumini kwa kusema kifo cha Padri Mushi hakikutokana
na mapenzi ya Mungu bali kimetokana na magaidi waliokatiza uhai wake.
Kauli hiyo iliibua kelele za shangwe kutoka kwa waumini hao ambao waliendeleza kelele za kumzomea Waziri Aboud.
Askofu Shao alisema wakati huu si wa kukumbatia maovu na kusisitiza
kifo cha Padri Mushi hakikutokana na mapenzi ya Mungu, bali kimefanywa
na watu wakatili waliokatiza maisha yake.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibrod Slaa wakati akitoa salamu za chama chake, alisema kuwa taifa
liko katika hatari ya kusambaratika kwani kuna viashiria vya wazi
vinavyoonesha kuwa tuko katika wakati mgumu.
Alivitaja viashiria hivyo kuwa ni pamoja na kuuawa kwa kupigwa risasi
Padri Mushi, kupigwa risasi kwa Padri Ambrose Mkenda, kuuawa kwa
mchungaji Geita katika mzozo wa kuchinja, kuuawa kwa mwandishi wa
habari, Daudi Mwangosi na matukio mengine.
Dk. Slaa alitofautiana na kauli ya Rais Jakaya Kikwete kutaka kuleta
wachunguzi kutoka nje, akisema hatua hiyo ni sawa na kushughulikia tawi
badala ya kukata shina na mizizi.
Mbali ya matukio hayo, ibada ya kumuaga padri Mushi ilianza saa mbili
asubuhi na kufanyika katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, katika eneo la
Minara Miwili mjini hapa.
Pengo aongoza misa
Misa hiyo iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam,
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na kufuatiwa na maandamano yaliyokuwa
na ulinzi mkali kuelekea katika makaburi ya Kitope.
Maaskofu wengine waliohudhuria ni Balozi wa Baba Mtakatifu, Askofu
Mkuu Frachesco Padilah, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania,
Tarcius Ngalalekumtwa, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora, Paulo
Ruzoka, ambaye pia ni msimamizi wa kitume wa Jimbo la Kigoma na Askofu
wa Mahenge, Agapitus Ndorobo.
Wengine ni Askofu wa Tanga, Anthony Banzi, Askofu Renatus Mkwande wa
Bunda, Askofu Gervas Nyaisonga wa Dodoma, Askofu Damian Dallu wa Geita
na mwenyeji wao, Askofu Agustino Shao wa Zanzibar, akiwamo na Makamu
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mt. Augustine, Dk. Charles Kitima.
Maaskofu wengine waliohudhuria ni pamoja na Askofu Mstaafu wa
Anglikana Zanzibar John Ramadhan, Askofu Mkuu wa KKKT Tanzania, Dk.
Alex Malasusa akiwakilishwa na wachungaji, Charles Mgena na George Fupe.
Viongozi wa serikali waliongozwa na Rais wa Zanzibar, Ali Mohammed
Shein, Makamu wa Kwanza, Maalim Seif na mawaziri Mwinyi Makame,
Mohammed Aboud na Said Mbaruku.
CHADEMA iliwakilishwa na Dk. Wilbrod Slaa na James Mbatia (NCCR-Mageuzi).
Hotuba ya Baba Mtakatifu yaliza wengi
Hotuba ya Baba Mtakatifu, Benedict wa 16 iliyosomwa na Balozi wake, Padilah, iliwaliza wengi.
Baba Mtakatifu pamoja na kueleza kushitushwa kwake na mauaji ya Padri
Mushi, alisema hata kama watumishi wake watashambuliwa, watatakiwa
kujibu kwa upendo na kufanya kazi za utume kwa nguvu kwa kuwapenda hata
maadui.
Alisema kifo cha Padri Mushi kisiwakatishe tamaa ya kufanya utume wao.
“Watu fulani wamemkatisha maisha yake. Hatuelewi kwa nini mtu mwema
ananyimwa nafasi ya kutimiza kazi yake. Naamini Yesu atatusaidia
kutimiza, maana hili ni jaribio la imani yetu,” imesema sehemu ya hotuba
hiyo.
Padri aliyejeruhiwa kwa risasi aibuka
Padri Ambrose Mkenda, aliyepigwa risasi na kujeruhiwa vibaya amepata
nafuu na kushiriki ibada ya misa ya kumuombea Padri Mushi, iliyofanyika
katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph jana jioni.
Kuhudhuria kwa Padri Mkenda katika ibada hiyo maalumu kulitangazwa na
Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius
Nzigirwa, ambaye alikuwa akiiongoza.
Hatua ya kumtambulisha Padri Mkenda kuhudhuria ibada hiyo naye
akasimama, ilishangiliwa na waumini wa kanisa hilo waliohudhuria misa
hiyo kwa kupiga makofi na vigelegele.
No comments:
Post a Comment