MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi,
imemuhukumu Abisai Joseph (40) mkazi wa Mtaa wa Kigamboni, Kata ya
Shanwe mjini hapa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumbaka mtoto
wake wa miaka sita.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya
wilaya hiyo, Chiganga Tengwa ambapo Joseph anadaiwa kutenda kosa hilo
Desemba 18 mwaka jana, saa tano usiku akiwa nyumbani kwake.
Awali, Mwendesha Mashtaka Ally Mbwijo, aliieleza mahakama kuwa siku
hiyo ya tukio Joseph alimbaka mwanaye baada ya kumvizia wakati alipo
toka kujisaidia haja ndogo.
Alidai kuwa baada ya kumkuta nje, alimvua nguo kisha alimweka sehemu
ya mapaja yake na kuanza kumfanyia kitendo hicho, na kwamba pamoja na
mtoto huyo kupiga kelele za kuomba msaada, mama yake aliyekuwa amelala
ndani hakuweza kusikia.
Mbwijo aliongeza kuwa baada ya kumaliza kufanyiwa kitendo hicho,
mtoto huyo aliingia ndani akilia, hali iliyomfanya mama yake amuulize,
lakini baba yake alijibu upesi kuwa alimkuta nje akibakwa na balozi
wao wa nyumba kumi.
Alidai kuwa baada ya maelezo hayo, mama wa mtoto, Sauda Rajabu
alikwenda kwa majirani kuwapa taarifa ya kitendo hicho, lakini
walimshauri ende kutoa taarifa polisi.
“Akiwa hapo polisi mtoto huyo alikana kubakwa na balozi wao, bali alisema aliyembaka ni baba yake mzazi,” alidai.
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi wanne
akiwemo mtoto mwenyewe aliyebakwa na mshtakiwa hakuwa na shahidi
yeyote.
Hakimu Chiganga katika hukumu hiyo alisema mahakama imeridhika na
ushahidi uliotolewa na kwamba imemtia hatiani mshtakiwa kwa kuvunja
sheria namba 130 (1) (e) na 131 (3) kifungu cha marekebisho ya sheria
ya mwaka 2009.
Alisema kutokana na kosa hilo mahakama inamuhukumu Joseph kifungo cha
maisha jela ili liwe funzo kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linamshikilia
Asajile Mwamtima (46) mkazi wa Kijiji cha Syukula, Wilaya ya Rungwe kwa
tuhuma za kumuingilia kimwili mtoto wake wa miaka 13 (jina
linahifadhiwa) mwenye ugonjwa wa kifafa.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Barakael Masaki alisema
mtuhumiwa alimuingila kimwili mtoto huyo ambaye inadaiwa aliacha shule
akiwa darasa la tano mwaka 2011 kutokana na ugonjwa huo.
Alisema kuwa mtuhumiwa alimvizia mtoto huyo akiwa jikoni anapika
chakula na kisha kumuingilia wakati mama mzazi, Tumikigwe Samalinga
akiwa katika Kijiji cha Kiwira kumuuguza mgonjwa.
Masaki alisema taratibu za kumfikisha mtuhumiwa mahakamani zinafanyika.
Katika tukio lingine, Kamanda Masaki alisema watu watatu wa familia
moja wamefariki dunia baada nyumba waliyokuwa wanaishi kugongwa na
gari.
Alisema tukio hilo limetokea katika Kijiji cha Ilongo, Wilaya ya
Mbarali likihusisha gari namba T 578 ALS lililokuwa likiendeshwa na
dereva ambaye hakufahamika, ambalo liligonga kwa nyuma gari aina ya
Scania lenye namba T 959 ASC lililokuwa likiendeshwa na Juhud Saimon na
kisha gari hilo kugonga nyumba na kusababisha vifo hivyo.
Aliwataja waliokufa kuwa ni Asia Yahaya (52), Abubakari Yahaya (8)
ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Ilongo na
Fatuma Yahaya (6) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza katika
Shule ya Msingi Ilongo.
Kamanda aliongeza kuwa watu wengine watatu walijeruhiwa akiwemo raia
wa Zambia ambaye ni msindikizaji wa gari lililosababisha ajali.
Habari na Walter Mguluchuma, Katavi wa Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment