SERIKALI imetakiwa kuacha kukurupuka kufuta matokeo ya kidato
cha nne mwaka 2012 kutokana na sababu za msingi za kufeli kwa wanafunzi
hao zinafahamika.
Hayo yalielezwa jana jijini Dar es Salaam na muungano wa asasi tano za
kiraia uliowakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Elizabeth
Missokia.
Asasi zilizotoa tamko la pamoja huku zikipendekeza njia sahihi ya
serikali kuwekeza katika elimu ni pamoja na Hakielimu yenyewe, Policy
forum, Sikika, TenMet na TGNP.
Kwa niaba ya mitandao hiyo mkurugenzi huyo alisema hakukuwa na haja ya
kufuta matokeo hayo na kufanya maboresho kwa kuwa sababu
zilizosababisha kufeli kwa wanafunzi zinajulikana na si kama serikali
inavyodai kwa sasa.
Missokia alisema kabla ya serikali kutoa uamuzi huo ilitakiwa kuweka
wazi mapendekezo ya Tume ya Waziri Mkuu iliyoundwa kuchunguza matokeo
hayo ili wadau wa elimu wapate fursa ya kuona sababu zilizochangia
kushuka kwa ufaulu katika mitihani hiyo.
“Kwa kufuta matokeo hayo bila wadau kujua sababu na kutoa mchango wao
inawaaminisha Watanzania kwamba sababu nyingine hata kama zipo
ziliathiri kwa kiwango kidogo matokeo hayo na suala la upangaji wa
madaraja kuonekana ni sababu kubwa zaidi kuliko nyingine,” alisema
Missokia.
Alisema hiyo sio sababu kwani matokeo ya kidato cha nne yaliyopita
huku akiyataja ya mwaka 2009 yalikuwa asilimia 27.5 ya watahiniwa
waliopata daraja sifuri, mwaka 2010 sifuri walikuwa 49.6 na mwaka 2011
asilimia 46.4 ambayo ni matokeo mabaya pia.
Alisema kwa mtiririko huo wa matokeo ni lazima kulikuwa na sababu
kubwa zaidi iliyochangia kushuka kwa ufaulu na kwamba hakuna uhusiano
wa moja kwa moja kati ya kubadili utaratibu wa kupanga matokeo na
ufaulu duni wa 2012.
Ilielezwa kuwa sababu nyingine ni kutokuwa na walimu wa kutosha hasa
kwa masomo ya sayansi; shule kuwa na upungufu mkubwa wa vitabu na vifaa
mbalimbali vya kujifunzia na kufundishia; bajeti ya maendeleo shuleni
kuwa ndogo; ruzuku mashuleni kufika ikiwa pungufu na wakati mwingine
ikiwa imechelewa; mihtasari ya kufundishia ina mkanganyiko mkubwa; na
huku mtaala mpya wa mwaka 2005 ukiwa mgeni kwa walimu walio wengi.
“Msingi mbovu wa lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo lugha ya
mawasiliano darasani; walimu kutokuwa na hamasa ya kufundisha kutokana
na madai ya muda mrefu na kufanya kazi katika mazingira magumu sambamba
na kukosekana kwa mafunzo kazini ya kuwaimarisha katika ufundishaji wao;
na hamasa ndogo miongoni mwa wazazi katika kufuatilia malezi ya watoto
wao,” alisema Missokia.
Hata hivyo alieleza kuwa kuandaliwa upya kwa matokeo hayo, serikali
inatakiwa ikumbuke kuna athari mbalimbali ambazo zitatokea ikiwa ni
pamoja na baadhi ya wanafunzi ambao walijiua baada ya kupata matokeo
mabaya.
“Sasa endapo watapata alama za juu nani atakayetakiwa kuwajibishwa kwa hilo?”
Pia kuna baadhi ya wanafunzi na wazazi wameshafanya maamuzi
mbalimbali, pamoja na waliokata tamaa na wamepata madhara makubwa
kisaikolojia na wengine kukubali kurudia mitihani na kuhoji serikali
itatoa fidia gani.
Pia waliwashukia NECTA kutokana na kukanusha kutumika kwa utaratibu
mpya wa upangaji wa madaraja huku wakihoji hivyo iliwadanganya
Watanzania.
Asasi hizo pia zilieleza kuwa kwa kuwa serikali imeamua kufuta matokeo
hayo na hatimaye kupangwa upya kwa utaratibu wa mwaka 2011 zilishauri
zoezi hilo kufanyika kwa uwazi kwa kushirikisha wadau wengine wa elimu
ili kujiridhisha na uhalali wa alama za wanafunzi zitakazokuwa
zinarekebishwa na siyo uchakachuaji katika njia za urekebishaji na
upangaji wa matokeo katika madaraja.
CHANZO TANZANIA DAIMA.
No comments:
Post a Comment