MAHAKAMA ya Rufaa nchini leo inatarajia kutoa uamuzi rufaa
iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Dk. Eliezer Feleshi, dhidi
ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna
Msaidizi, Abdallah Zombe, wa kuifuta au kutoifuta rufaa iliyokatwa na
DPP baada ya jicho la mahakama kuona hati ya kukatia rufaa ina dosari.
Sambamba na hilo, pia Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo
inatarajia kutoa uamuzi wa kuifuta au kutoifuta kesi ya tuhuma za ugaidi
za kutaka kumteka mhariri wa gazeti la Mwananchi, Denis Msaki,
inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA),Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph.
Mahakama kuu iliombwa ifanyie mapitio majalada ya kesi ya msingi
iliyoko mahakama ya Kisutu inayomkabili Lwakatare iliyofunguliwa
mahakamani hapo mbele ya Jaji Lawrance Kaduri na washtakiwa hao, ambapo
lilisikilizwa Aprili 15 mwaka huu na mawakili wa Lwakatare, Peter
Kibatara, Tundu Lissu na Mabere Marando walidai kitendo alichofanya
Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) hakikuwa cha lazima.
Kwamba licha ya mkurugenzi huyo kuwa na mamlaka ya kufuta kesi, lakini
anapofanya hivyo lazima aonyeshe amefuta kwa maslahi ya umma, kutafuta
haki au pengine kuzuia mahakama isidhalilike na hukumu ambayo
ingetolewa.
Mawakili hao walidai kuwa kesi iliyofutwa na kurejeshwa tena Kisutu
ilikuwa ni matumizi mabaya ya mamlaka ya DPP, hivyo kuiomba Mahakama Kuu
kupitia upya mwenendo wa kesi namba 37/2013 iliyofunguliwa Kisutu kwani
ilifunguliwa kwa nia ya kumdhalilisha mtuhumiwa.
Walihoji iliwezekanaje kufuta kesi na kuifungua ndani ya muda mfupi, kwamba walipata wapi ushahidi mwingine mpya.
Mawakili hao wa utetezi wanaiomba Mahakama Kuu ifanye yafuatayo:
Kwanza, ipitie mwenendo wa kesi zote mbili, namba 37/2013 na 6/2013 ili kujua kama zina hoja ya msingi, halali au la.
Pili, wanaomba mahakama iamrishe kuwa mwenendo wa kesi namba 6 urudi
katika kesi namba 37, ili mahakama ya Kisutu iweze kutoa hukumu kutokana
na mambo yaliyokuwa yanabishaniwa kisheria.
Tatu, wanaiomba Mahakama Kuu kuingilia mchakato wa ‘nole’ (hawana
hatia) iliyotolewa na DPP kwa muda mfupi kisha kumtia mtuhumiwa hatiani,
kitu ambacho ni kinyume kabisa cha madaraka ya DPP.
Nakuongeza kuwa anaiomba mahakama kuu iifute kesi ya msingi
inayowakabili washtakiwa hao kwa sababu makosa ya pili, tatu na nne
hayaonyeshi nia ya washtakiwa hao kutenda makosa ya ugaidi; alidai kuwa
hoja hizo zimeletwa wakati usio sahihi kwani kesi ya msingi iko katika
hatua za uchunguzi, upelelezi bado haujakamilika.
Kwa upande wao mawakili wanaomwakilisha DPP, Prudence Rweyongeza na
Ponsian Lukosi wakijibu hoja za mawakili wa washtakiwa walipangua hoja
ambazo zilidai DPP alitumia madaraka yake vibaya kuifuta kesi Na.
37/2013 na akazitaja sababu zilizosababisha aifute kesi hiyo na kufungua
kesi mpya Na. 6/2013 Machi 20, mwaka huu, kwa kuwa mashtaka ni yale
yale.
Rweyongeza alitaja sababu ya kwanza iliyofanya DPP aifute kesi Na. 37
/2013 iliyofunguliwa Machi 18 mwaka huu, kuwa ni uongozi wa Mahakama ya
Kisutu kukosea na kuifungua kesi hiyo katika jalada la kesi
zinazoendeshwa katika mahakama za chini badala ya kuisajili kesi hiyo
katika rejista ya kesi zinazopaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu.
Pili, ni kwamba hakimu aliyeisikiliza kesi hiyo, Emilius Mchauru,
alikosea kuwaruhusu washtakiwa hao kujibu mashtaka wakati Mahakama ya
Kisutu haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza kesi hiyo ya ugaidi.
“Hivyo basi upande wa jamhuri tunasisitiza kuwa uamuzi wa DPP wa
kuifuta kesi ile ulikuwa wa haki ambao ulikidhi matakwa ya kifungu cha
nane cha Sheria ya Uendeshaji wa Mashtaka ya mwaka 2008,” alidai
Rweyongeza.
Aprili 22 mwaka huu, jopo la majaji wa Mahakama ya Rufaa linaloongozwa
na Jaji Edward Rutangakwa na Mbarouk Mbarouk na Milla lilibaini dosari
katika hati ya kukata rufaa na kwamba hati hiyo ilisomeka kuwa Jaji
Salum Massati ambaye ndiye alitoa hukumu ya mahakama kuu na
kuwamwachilia huru Zombe na wenzake walimtambulisha kuwa ni jaji wa
Mahakama ya Rufaa, badala ya kuandika kuwa wakati huo Jaji Massati
alikuwa ni jaji wa mahakama kuu na sasa ni jaji wa Mahakama ya Rufaa na
kwa dosari hiyo jopo hilo lilisema Mahakama ya Rufaa haiwezi kusikiliza
rufaa ambayo hukumu yake imetolewa na jaji mwenzao wa Mahakama ya Rufaa
na hivyo rufaa hiyo ikashindwa kusikilizwa hiyo Aprili 22 mwaka huu, na
likaahidi kwenda kuandaa uamuzi wake kuhusu kubainika kwa dosari hiyo
ambapo uamuzi wake wanautoa leo.
No comments:
Post a Comment