WAKULIMA wawili wilayani Kiteto, wamenusurika kuuawa na wafugaji
jamii ya Kimasai baada ya kuibuka mapigano kufuatia ng’ombe kula mazao
shambani.
Wakulima hao walionusurika kuuawa ni Samweli Malima (35) na Sanagali Athumani (29), wote wakazi wa Njutaa.
Akizungumza na Tanzania Daima jana hospitalini walipolazwa majeruhi,
baba mzazi wa majeruhi hao, Waziri Mtambo (55) alisema tukio hilo
lilitokea Mei 15, majira ya saa 7 mchana wakati vijana hao wakiwa
shambani wakivuna mahindi.
Alisema vijana hao walipofika shambani waliwakuta ng’ombe wanakula
mazao ndipo walipowauliza vijana wachungaji waliokuwa wakichunga ng’ombe
hao na ndipo ukatokea ubishani.
Mtambo alisema baada ya muda mfupi walitokea Wamasai sita kwenye
kibanda cha shambani ambacho Malima na Athumani kipindi hicho walikuwa
wamepumzika na kuomba na wao kupumzika wakidai wamechoka baada ya
kutembea umbali mrefu wakichunga ng’ombe ambao hawakuwa nao.
“Baada ya muda wakaongezeka tena Wamasai wengine na kuanza kuwachoma
choma na sime ubavuni huku wakihoji kwanini wanazuia ng’ombe wasile
chakula,” aliongeza.Alisema kutokana na hali hiyo, vijana hao walianza
kujitetea, lakini walizidiwa nguvu na Athumani alizimia ndipo
walipokimbia.
Mtambo alisema vijana hao waliokolewa na wapita njia ambao walitoa
taarifa kijijini na wananchi kwenda mashambani ambako waliwakuta
wametapakaa damu huku wakiwa wamepoteza baadhi ya viungo vya mwili.
“Athumani ambaye hali yake ni mbaya amechanwa na sime kichwani na
kupasua mfupa wa fuvu, ametobolewa kwapani na sime, paji la uso kushoto
karibu na jicho, amechunwa ngozi hadi usawa wa sikio na sime na Samweli
Malima amekatwa dole gumba la mkono wa kulia, amejeruhiwa kichwani kwa
sime na sehemu mbalimbali mwilini,” alifafanua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa alikiri kuwepo kwa
tukio hilo na kwamba tayari askari wameagizwa kwenda kudhibiti hali
katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment