MREMBO atakayefanikiwa kutwaa taji la kitongoji cha Kigamboni mwaka huu ‘Redd’s Miss Kigamboni 2013’ katika shindano litakalofanyika leo usiku kwenye Ukumbi wa Navy Beach, Kigamboni atajinyakulia kitita cha Sh 500,000.
Maandalizi ya shindano hilo yamekamilika na warembo 12 kutoka sehemu mbalimbali hapa jijini Dar es Salaam, watapanda jukwaani kuwania taji hilo.
Akizungumza na gazeti hili jana, mratibu wa shindano hilo, Somoe Ng’itu, alisema mrembo atakayeshika nafasi ya pili katika shindano hilo, atapata Sh 300,000, mshindi wa tatu Sh 250,000 huku wawili watakaotangazwa kushika nafasi ya nne na ya tano, kila mmoja akiondoka na Sh 200,000.
Somoe alisema kuwa warembo wengine saba waliobakia kila mmoja atapata kifuta jasho cha Sh 100,000.
“Najua wote ni warembo na wana sifa za kutwaa taji hilo, lakini ni msichana mmoja tu ndiye atakayetangazwa mshindi wa shindano hilo, tunawaomba wadau wa sanaa ya urembo kuja kushuhudia safari ya Redd’s Miss Tanzania, ikianzia Kigamboni leo,” alisema Somoe.
Aliitaja bendi ya FM Academia maarufu kama Wazee wa Ngwasuma kwamba itatumbuiza katika shindano hilo. Kiingilio cha viti maalum ni Sh 10,000 na viti vya kawaida ni Sh 5,000.
No comments:
Post a Comment