Amri Kiemba akiongea na Rais Kikwete kabla ya mechi ya wabunge wa Simba na Yanga.
KIUNGO wa Taifa Stars, Amri Kiemba, amejikuta katika wakati mgumu baada ya kukabidhiwa majukumu makubwa na Rais Jakaya Kikwete.
Hatua hiyo inakuja wakati ambao Stars imebakiza siku tatu kabla ya
kushuka katika Uwanja wa Taifa jijini Dar, kuumana na Uganda katika
mchezo wa kuwania nafasi ya kushiriki Fainali za Kombe la
Mataifa ya
Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan).
Kiemba alikabidhiwa majukumu hayo mara baada ya kukutana na Rais
Kikwete mwishoni wa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam wakati wa Tamasha la Matumaini ambapo kiungo huyo aliungana na
timu ya Wabunge wa Simba.
Wakati Rais Kikwete akisalimiana na kikosi hicho cha wabunge,
alikutana na kiungo huyo ambapo mara baada ya kufanya hivyo, alimtaka
Kiemba kuongeza juhudi zaidi huku akimweleza kuwa anafuatilia kila kitu
juu ya soka la Tanzania.
Rais Kikwete hakuishia hapo, alimtaka Kiemba kuhakikisha anawahimiza
nyota wenzake waliopo katika kikosi cha Stars kuhakikisha wanafanya
vizuri katika michezo iliyo mbele yao huku akimwambia hataki kusikia
lingine lolote zaidi ya ushindi.
“Ongeza juhudi, unafanya vizuri, lakini ongeza bidii, nataka
ukawaambie na wenzio mhakikishe mnafanya vizuri zaidi, nawafuatilia,
nataka kuona mnafanya vizuri katika michezo yenu yote, nataka kusikia
ushindi tu sasa,” alisema Kikwete.
Wakati wote Kiemba alikuwa akitikisa kichwa na kuitikia “sawa, sawa”, kuonyesha alielewa alichokuwa anaelezwa na Rais Kikwete.
Kabla ya hapo, Rais Kikwete alikuwa amesalimiana na beki Shomari
Kapombe ambaye alikuwa katika mstari huo wa wachezaji wa Wabunge wa
Simba.
Kwa upande wa Wabunge wa Yanga, wachezaji walioungana nao walikuwa ni
Ally Mustapha ‘Barthez’ pamoja na beki wa kati wa Yanga, Kelvin
Yondani.
Credit GLP
No comments:
Post a Comment