Na Dixon Busagaga, Moshi
KESI ya kutorosha wanafunzi wawili, inayomkabili Jean Felix
Bamana, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imeahirishwa
kutokana
na mashahidi wa upande wa Mashtaka kushindwa kufika mahakamani.
Mwendesha mashtaka wakili wa Serikali Abdalah Chavula, aliiambia
mahakama kuwa shahidi wa sita katika kesi hiyo Koplo Mfume, mwenye
namba AE2524 wa kituo cha polisi Bomang’ombe wilayani Hai, ameshindwa
kufika mahakamani hapo kutokana na kuwa na majukumu mengine.
Chavula aliiambia mahakama shahidi wa saba katika kesi hiyo Media Juma
kutoka Dar es Salaam alijulishwa kuhusu kuhitajika kutoa ushahidi
mahakamani hapo kwa njia ya simu, lakini hadi mahakama inaanza
kusikiliza kesi hiyo jana, hakukuwa na mawasiliano yoyote kati yake na
shahidi huyo na kwamba shahidi wa nane, Sajenti Mwajuma, alipata
dharura ya kikazi.
Hata hivyo, mshtakiwa kupitia kwa wakili wake, Erick Gabriel,
alionyesha kutoridhika na maamuzi ya kuahirishwa kwa kesi hiyo
kutokana
na madai ya mashahidi kutofika mahakamani huku akiwasilisha pingamizi
la kukosekana kwa shahidi namba nane, Sajenti Mwajuma ambaye alifika
mahakamani hapo na kutoweka muda mfupi kabla mahakama haijaanza.
Wakili Gabriel aliiambia mahakama hiyo kuwa madai kwamba Sajenti
Mwajuma alishindwa kufika mahakamani hapo kutokana na kupata dharura
za kikazi ni kuipotosha mahakama kwani shahidi huyo alionekana nje ya
mahakama muda mfupi kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa.
“Mheshimiwa hakimu, naomba kuwasilisha pingamizi katika kile
kinachodaiwa kuwa ni kushindwa kufika kwa sajenti Mwajuma, tunaomba
kuieleza mahakama yako tukufu kuwa shahidi huyo alionekana muda mfupi
katika eneo la mahakama kabla ya kesi kuanza, hivyo
hatuelewi ni kwa nini upande wa jamhuri umeshindwa kuhakikisha anafika
na kutoa ushahidi wake,” alisema Gabriel.
Kutokana na madai hayo mwendesha mashtaka wa serikali, Wakili Chavula,
aliiambia mahakama kuwa huenda kuonekana kwa Sajenti katika maeneo ya
mahakama ilikuwa ni sehemu ya kumalizia maombi ya ruhusa.
Awali shahidi wa tano katika kesi hiyo Angela Swai (17) aliileza
mahakama ya hakimu mkazi Moshi, mbele ya hakimu Naomi Mwerinde namna
mshtakiwa alivyomlazimisha kufanya naye mapenzi bila
kutumia kondomu.
Katika kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa Aprili 13, mwaka huu, inadaiwa
kuwa mshtakiwa huyo ambaye alitajwa mahakamani hapo kuwa ni mchungaji
katika kanisa la TAG Mikocheni la Mama Getrude Lwakatare, inadaiwa
kuwa mnamo Februari 14, mwaka huu, aliwarubuni wanafunzi wawili, Angel
Swai (19) na mwenzake mwenye umri wa miaka 17 jina linahifadhiwa kwa
madai ya kuwasomesha nje ya nchi.
Bamana anashtakiwa kwa makosa mawili ya kutorosha wanafunzi, kinyume
cha sheria ya Jamhuri ya Tanzania chini ya sheria namba 6 ya mwaka
2008, ibara ya 4, kifungu cha 5, kifungu kidogo 4 (i) a.
Kesi hiyo itasikilizwa tena Agosti 30 katika mahakama ya hakimu mkazi
Moshi, baada ya upande wa mashtaka kuahidi kuwaleta mashahidi hao
mahakamani hapo kutoa ushahidi wao.
No comments:
Post a Comment