Na Ashura Jumapili, Kagera
ZAIDI ya wazee 300 huuawa nchini kila mwaka kutokana na imani za kishirikina na umaskini.
Hayo yalibainishwa na mratibu wa taasisi ya Saidia Wazee Karagwe
(Sawaka), Livingstone Byekwaso, katika warsha ya siku moja yalioendeshwa
na chama hicho kwa waandishi wa habari mkoani hapa.
Alisema, “Kila mwaka wazee zaidi ya 300 wanauawa nchini kwa tuhuma za uchawi.
“Pia hunyang’anywa mali zao na hii inatokana na umaskini uliopo kwa
baadhi ya vijana na ukosefu wa elimu ndani ya jamii,” alisema.
Alisema wazee hao zaidi ya 300, wamekuwa wakiuawa hasa katika mikoa ya
Kanda ya Ziwa, Kagera, Simiyu, Shinyanga, Geita, Mwanza na Tabora.
Halikadhalika wazee hao wamekuwa wakinyanyaswa zaidi katika mkoa wa Kagera ambapo wazee wamekuwa wakifyekewa mashamba yao.
Alisema wazee wamekuwa wakikabiliwa na matatizo mbali mbali, ikiwemo
maagizo yanayotolewa na serikali hayapewi uzito wowote kama ya kutibiwa
bure katika hospitali za umma.
Kwa mujibu wa Byekwaso asilimia 54, sawa na watoto yatima milioni
mbili wamekuwa wakihudumiwa na wazee baada ya wazazi wao kufariki kwa
ugonjwa wa ukumwi, hivyo kuwaongezea mzigo wazee hao.
Halikadhalika alisema asilimia nne ya wazee hapa nchini ndiyo walio
kwenye mfumo wa malipo ya pensheni na asilimi 96 wanaobaki hawamo katika
mfumo huo, jambo ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa wazee kuishi
katika mazingira magumu na kushidwa kumudu gharama za kupata mahitaji
yao ya kila siku kama chakula, malazi na mavazi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Shirika la Tanzania Social Protect
Network, Ramadhan Msoka, katika Ripoti ya Shirika la Haki za Binadamu
mwaka 2011, inaonesha kuwa jumla ya wazee 689 waliuawa kwa imani za
kishirikina.
No comments:
Post a Comment