Vurugu zilizotokea Bungeni juzi na jana wakati wa mjadala wa
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013
zimeacha mashaka kama kweli nchi yetu itaweza kupata Katiba Mpya ya
kutupeleka kule tunakotaka kwenda.
Vurugu hizo ni mwendelezo wa hali ya kutovumiliana miongoni mwa wabunge kutokana na kuweka mbele itikadi na misimamo ya vyama vya siasa badala ya kutanguliza masilahi ya taifa.
Vurugu hizo ni mwendelezo wa hali ya kutovumiliana miongoni mwa wabunge kutokana na kuweka mbele itikadi na misimamo ya vyama vya siasa badala ya kutanguliza masilahi ya taifa.
Tunadiriki kusema kwamba kama hautatokea muujiza katika muda mfupi ujao, hapa tulipofika ndio utakuwa mwisho wa maono na ndoto za Watanzania za kupata Katiba Mpya waliokuwa wakiitafuta kwa muda mrefu sasa.
Moja ya matatizo yanayochochea hali ya kutosikilizana wakati wa mijadala ya muswada huo ndani ya Bunge ni kila kambi kutaka kupata kila kitu, hivyo kushindwa kukubali ukweli kwamba katika hali ya mapatano kama hayo ya mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya kuna kupata hili na kukosa lile.
Matukio yaliyotokea Bungeni mjini Dodoma siku mbili mfululizo sio tu yanatishia kutopatikana mwarobaini wa tofauti zilizopo katika kambi hizo za kiitikadi, bali pia upatikanaji wa Katiba Mpya na katika wakati uliopangwa.
Wabunge kutoka vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na
CUF walitoka nje ya Ukumbi wa Bunge jana na juzi wakitaka muswada huo
uondolewe Bungeni kwa madai kwamba Wazanzibari hawakupewa fursa stahiki
kuutolea maoni. Upande wa Serikali na chama tawala ulishikilia msimamo
kwamba muswada huo hautaondolewa Bungeni kwa sababu wadau wote
walishirikishwa ipasavyo.
Wakati huohuo, mbunge wa kambi ya upinzani alisoma vifungu vya muswada huo ambavyo alidai vilichomekwa na Serikali kinyemela na kwamba havikuwa katika muswada waliopelekewa wabunge.
Kila kambi iliituhumu nyingine kwa kukwamisha mjadala wa muswada huo ili Katiba Mpya isipatikane. Mtafaruku zaidi ulitokea jana wakati Naibu Spika, Job Ndugai alipomwamuru Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge kwa kukaidi maagizo yake ya kukaa chini. Ghasia kubwa zilizuka kabla ya kiongozi huyo kutolewa nje, huku akifuatana na wabunge wengi wa upinzani.
Kama ilivyokuwa juzi, wabunge wa CCM jana pia waliendelea na mjadala wa muswada huo mara baada ya wabunge wa upinzani kutoka nje.
Hata hivyo, badala ya kujadili muswada huo, wabunge wengi wa CCM walijielekeza katika kuwapiga vijembe wabunge wa upinzani waliotoka nje, hivyo kusababisha hali inayoweza kuongeza msuguano na kuweka mazingira ya kutowawezesha wabunge kuwa kitu kimoja katika kujadili muswada huo kwa kina na umakini kwa lengo la kupata msimamo wa pamoja.
Sisi tunadhani zinahitajika nguvu za ziada kulirudisha Bunge ndani ya mstari kama tunataka kupata muswada utakaokubalika.Kuna msemo usemao wengi wape, lakini wachache nao wasikilizwe.
Maana ya msemo huo ni kwamba sio lazima walio wengi wakati wote kuwa na maoni sahihi, bali pia kuna wakati walio wachache nao huwa na maoni sahihi.
Kwa mfano, ukweli wa usemi huo tuliushuhudia wakati Tume ya Nyalali kuhusu kuwapo au kutokuwapo vyama vingi ilipotoa ripoti kwamba zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania waliotoa maoni yao walitaka utawala wa chama kimoja. Pamoja na hali hiyo, Tume hiyo ilipendekeza uwapo wa vyama vingi na hatimaye ikawa hivyo.
CHANZO CHA HABARI NA MWANANCHI
No comments:
Post a Comment