Bunge la Kenya limeitisha kikao
cha dharura kujadili kujiondoa kwa nchi hiyo kama mwanachama wa Mahakama
ya kimataifa ya Uhalifu ICC.
Naibu wa Rais wa Kenya William Ruto alikuwa
amepangiwa kufika mbele ya mahakama hiyo ya ICC wiki ijayo kujibu
mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu. Naye rais Uhuru Kenyatta
anatarajiwa kufika mbele ya mahakama hiyo mwezi Novemba.Uamuzi
huu umechukuliwa kutokana na shinikizo kutoka kwa wabunge na wanachama
wa chama kinachotawala cha Jubilee kutaka kuondolewa mashtaka
yanayowakabili viongozi Uhuru Kenyatta na William Ruto.
Naibu wa Spika Joyce Laboso amepanga kikao hicho
kufanyika Siku ya Alhamisi. Hata hivyo hata ikiwa bunge hilo
litapitisha hoja hiyo, kujiondoa kama mwanachama wa ICC, ni uamuzi ambao
lazima ufikishwe kwa wananchi katika kura ya maoni.
Baada ya kupita hapo ndipo itawasilishwa kwa
baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kupata idhini na kueleza sababu
kamili za kutaka kuchukua hatua hiyo, pamoja na kuwa wananchi wenyewe
wameamua.
Hata hivyo kwa mujibu wa sheria za mahakama hiyo
ya ICC, hata kama nchi itajiondoa kama mwanachama, kesi ambazo zilikuwa
tayari zimeshawasilishwa katika mahakama hiyo kuwahusu raia wa nchi
hiyo, lazima zitaendelea kusikizwa hadi mwisho na hukumu kutolewa.
Kwa hiyo hata ikiwa Kenya itajiondoa sasa,
viongozi wao Uhuru Kenyatta na William Ruto bado wanayo mashtaka ya
kujibu mbele ya mahakama ya ICC.
No comments:
Post a Comment