Dar es Salaam.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekusanya zaidi ya Sh4.7 bilioni, baada ya kuanzisha mfumo mpya wa kulipia ada za magari kwa njia ya mtandao.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekusanya zaidi ya Sh4.7 bilioni, baada ya kuanzisha mfumo mpya wa kulipia ada za magari kwa njia ya mtandao.
Kiasi hicho kimekusanywa ndani ya wiki tatu tangu
kuanza kwa mpango huo na kimeelezwa kuwa ni ongezeko la Sh1.1 bilioni ya
kiasi cha fedha zilizokuwa zikikusanywa katika kipindi kama hicho mwaka
jana.
Imeelezwa kuwa katika kipindi cha mwaka jana kabla ya kuanzishwa kwa utaratibu huo, TRA ilikusanya Sh3.6 bilioni.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi katika TRA, Richard Kayombo, alisema mfumo huo umesaidia kuondoa msongamano katika ofisi za mamlaka na kuepusha udanganyifu uliokuwa ukifanywa na vishoka.
“Kulikuwa na utapeli mwingi uliokuwa unafanywa na baadhi ya watu kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wetu. Kwa hiyo mfumo huu utasaidia kuondoa kero zote hizo,”alisema Kayombo.
Kwa mujibu wa Kayombo, utapeli huo ulisababisha watu kuchelewa kupata huduma na kwamba baadhi ya watu walikuwa na risiti za benki ambazo ni za kughushiwa.
Hata hivyo alisema wale wanaotaka kubadilisha umiliki wa magari, lazima waende ofisini kwa ajili ya uhakiki wa nyaraka.
Mkurugenzi huyo pia alisema wameanzisha mfumo mwingine wa kudhibiti mizigo bandarini.
Alisema mfumo huo ulioanza mwishoni mwa mwezi uliopita unalenga katika kupunguza kero na malalamiko kutoka kwa wadau na kuisaidia Serikali, ili isipoteze mapato.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, mfumo huo ulibuniwa kwa ushirikiano na kampuni ya Korea Kusini na maofisa wa TRA.
No comments:
Post a Comment