LICHA ya biashara ya dawa za kulevya kuzidi kushika kasi nchini,
serikali imeendelea na msimamo wake wa kuwagwaya kwa kutoweka majina
yao hadharani, ikidai kuwa kufanya hivyo ni kuwajengea mazingira ya
kutoroka.
Hata hivyo, utetezi huo unakinzana na kauli ya Rais Jakaya Kikwete
aliyowahi kukaririwa akisema kuwa anayo orodha ya wauza dawa hizo ambao
aliwapa muda wajirekebishe kabla ya kutaja majina yao.
Badala yake, serikali imesema sheria inayotumika sasa katika
kukabiliana na uhalifu wa dawa za kulevya nchini inatoa mwanya mkubwa
kwa wafanyabiashara hizo.
Akizungumza na jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema kuwa
serikali inawaalika wadau mbalimbali kutoa maoni yatakayoandaa sheria
mpya ya uthibiti wa dawa za kulevya.
Waziri Lukuvi alisema kutokana na ubovu wa sheria ya kupambana na dawa
za kulevya iliyotungwa mwaka 1995, mpaka sasa ni kesi moja tu kubwa
iliyotolewa uamuzi kati ya kesi 149 zilizoko mahakamani.
Alisema ni wakati wa wadau kutoa maoni ya kuundwa kwa sheria
itakayotoa hofu kwa mapambano ya dawa za kulevya hasa baada ya vyombo
vya ulinzi na usalama kutupiwa lawama juu ya kuzembea kukabiliana na
uhalifu huo nchini.
“Ni wakati wa kuipa tume ya kudhibiti dawa za kulevya uwezo wa
kupeleleza, kukamata na kushtaki badala ya mfumo uliopo sasa wa mtoa
taarifa kuwa mwingine, mkamataji mwingine na anayeshtaki mwingine,”
alisema.
Lukuvi aliongeza kuwa hali hiyo itawezekana kwa kuundwa kikosi kazi kitakachokuwa na uwezo wa kufanya mambo yote kwa pamoja.
Alifafanua kuwa ni wakati muafaka kuwa na mahakama maalum
itakayoshughulika na kesi za dawa ya kulevya au kuwe na muda maalumu wa
kusikiliza kesi hizo kama zilivyo kesi za uchaguzi.
Pia aligusia ubovu wa sheria iliyopo sasa akitolea mfano hukumu
inayotolewa kwa wafadhili na wafanyabiashara wa dawa za kulevya hasa
wanaokamatwa wakiwa na dawa za thamani kubwa.
“Hawa wafadhili hawana wasiwasi kwa kuwa hukumu yao ni suala la jaji
kuamua ama walipe sh milioni 10 au wahukumiwe kifo sasa huu ni uamuzi wa
jaji kuchagua moja na kwa kutozwa fedha hili kwao ni jambo dogo sana,”
alisema.
Kuhusu kuwataja wale wanaojihusisha na biashara hiyo, Lukuvi alisema
watuhumiwa wanaweza kuchukua tahadhari zaidi hivyo kusababisha kazi ya
kuwakamata iwe ngumu.
“Tukiwatangaza hadharani wengi watakimbia na sisi lengo letu ni kuzuia
uhalifu lakini mtambue kama majina yanayotajwa hayafanyiwi kazi
ipasavyo, basi kila siku kutakuwa na orodha ya watu wapya wanaokamatwa
na kisha kukosekana ushahidi,” aliongeza.
Lukuvi aliongeza kuwa kuna haja ya kutafuta vyanzo vingine vya mapato
kwa ajili ya kuiwezesha tume ya kudhibiti dawa za kulevya kufanya kazi
kwa uhakika badala ya kutegemea bajeti iliyotengwa na serikali kwa sasa.
“Tunataka hata wakiambiwa kuna muuzaji dawa huko Tanga muda huu wasifikirie sehenu ya kupata fedha kwa ajili ya kufuatilia.
“Hatuwezi kusema tutatenga sh bilioni 100 kwa kazi hiyo ila tuwe na
uhakika wa fedha zaidi kwa kuwa hatuwezi kupima ukubwa wa tatizo na
kukadiria ni kiasi gani tutatumia kwa mwaka,” alisema.
Alisema serikali itapokea maoni ya wadau mbalimbali juu ya sheria
itakayoweza kuboresha mapambano dhidi ya dawa za kulevya ambapo awamu ya
kwanza ya maoni hayo itaisha Oktoba 31 mwaka huu.
CHANZO TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment