NGEBE zilizodumu kwa siku kadhaa kwa mashabiki wa timu za Yanga
na Simba kwa kila mmoja kutamba ni zaidi, leo jioni zitapata jibu baada
ya filimbi ya mwisho kuamua nani mbabe kati ya miamba hiyo yenye utani
wa jadi tangu kuasisiwa kwao zaidi ya miaka 70 iliyopita.
Ingawa ligi hiyo iliyoanza Septemba 15, mwaka jana itahitimishwa kwa
timu zote 14 kushuka dimbani, mechi ya miamba hiyo miwili ndiyo imekuwa
gumzo kubwa likiambatana na visa, vibweka na vituko kama Simba kumkataa
mwamuzi na makomandoo kukesha wakilinda Uwanja wa Taifa.
Pamoja na Yanga kushuka dimbani tayari ikiwa na ubingwa mkononi ikiwa
na mechi mbili mkononi, bado inahitaji kushinda kulipa kisasi cha mabao
5-0 cha Mei 6, mwaka jana na kupamba sherehe za ubingwa baada ya filimbi
ya mwisho ya Martin Saanya kutoka Morogoro.
Tayari Yanga wametangaza kuwa bila ushindi katika mechi ya leo, hafla
ya ubingwa itakuwa imeingia dosari, hivyo wachezaji wametakiwa kushinda
ili kufanikisha hafla ya makabidhiano ya ubingwa kutoka kwa wadhamini wa
ligi hiyo, kampuni ya Vodacom-Tanzania.
Aidha, Yanga chini Mwenyekiti wake Yusuf Manji itakuwa ikisaka ushindi
kurejesha furaha kwa mashabiki wa timu hiyo kwani ndilo deni pekee kwa
uongozi huo uliochaguliwa Julai 15, mwaka jana, kupitia uchaguzi mdogo
baada ya kujiuzulu kwa Lloyd Nchunga baada ya kipigo cha 5-0.
Ni deni pekee baada ya Yanga chini ya Manji kufanikiwa kutetea ubingwa
wa Kombe la Kagame Julai 28, mwaka jana na kurejesha ubingwa wa Ligi
Kuu, hivyo kazi iliyobaki ni moja tu ya kulipa kisasi cha 5-0 baada ya
mechi ya kwanza katika msimu huu ya Oktoba 3, kwisha kwa sare ya bao
1-1.
Kwa kutambua umuhimu wa ushindi katika mechi ya leo, Yanga chini ya
Kocha wake Ernie Brandts inashuka dimbani ikitokea kisiwani Pemba
ilikokwenda kujifua kwa siku kadhaa kuhakikisha vijana wake wanashinda
mechi ya leo kuwapa raha wanachama, wapenzi na mashabiki wa timu hiyo
iliyobeba ubingwa wa 24 tangu mwaka 1965.
Ofisa habari wa Yanga, Baraka Kaziguto, alisema kikosi kilitarajiwa
kurejea jijini Dar es Salaam jana jioni kutokea Pemba walikoweka kambi
na kusema hawana hofu na mwamuzi Saanya kwani wako fiti kuhakikisha
wanashinda kulipa kisasi cha mabao 5-0 walicholimwa Mei 6, mwaka jana.
“Sisi ndio mabingwa, hivyo mechi ya kesho (leo) lazima tushinde na
hatuna hofu juu ya hilo, tuna uhakika wa kushinda hata kama Rage,
Hanspope na Julio watacheza,” alisema Kizuguto kwa kujiamini.
Wakati Kizuguto akisema hayo, naye ofisa habari wa Simba, Ezekiel
Kamwaga, alisema jana kwamba kikosi kimejizatiti vya kutosha na kuongeza
kuwa hata suala la kumgomea mwamuzi Saanya, limekwisha baada ya
viongozi wa Simba kukutana na TFF (Shirikisho la Soka Tanzania).
Kuhusu habari za kutimuliwa kambini kwa winga wao Mrisho Ngasa kwa
hofu ya kuhujumu kwa vile yu mbioni kujiunga na Yanga baada ya leo,
Kamwaga alisema jana kuwa mchezaji huyo bado yuko katika kikosi cha timu
hiyo ingawa suala la kupangwa ni uamuzi wa benchi la ufundi chini ya
Patrick Liewig.
“Mengi yanasemwa juu ya Ngasa, lengo ni kumuondoa mchezoni. Ngasa tuko
naye kambini hadi sasa ninapozungumza (jana), ingawa suala la kupwangwa
au kutocheza ni uamuzi wa benchi la ufundi tofauti na maneno yaliyoko
mitaani,” alisema Kamwaga.
Juu ya kikosi, Kamwaga alisema wachezaji wote watavalia mishipi myeusi
kama simanzi ya mchezaji mwenzao Patrick Mutesa Mafisango, aliyefariki
Mei 17 kwa ajali ya gari eneo la Veta, Dar es Salaam na mashabiki wenye
jezi namba 30 wametakiwa kuivaa kama ishara ya kutambua mchango wake.
Kwa upande wa ulinzi, jeshi la polisi kupitia kwa Kamanda wa Polisi
Kanda Maalum jijini Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema wamejipanga
kuhakikisha usalama unakuwa wa kiwango cha juu na kuwataka wananchi
kwenda uwanjani kwa wingi kwani usalama upo wa kutosha.
“Tumejipanga kikamilifu kuwakabili wote watakaoleta fujo hiyo kesho
(leo) na hatutaki kusikia watu wanatuambia sisi ni walizi kutoka Simba
au Yanga, tutalinda amani sisi wenyewe,” alisema Kova.
Hata hivyo, jeshi hilo lilianza jukumu hilo tangu jana kwa mashabiki
waliokuwa wamefurika kununua tiketi za mechi hiyo maeneo mbalimbali ya
jiji kama shule ya Benjamin Mkapa, Karume hasa baada ya mashabiki
kuanzisha vurugu wakihoji mantiki ya kukaa kwa muda mrefu kwenye foleni
bila kuzipata.
Kwa kukosa subira, baadhi ya mashabiki wenye hasira walivunja mlango
wa gari iliyokuwa ikiuza tiketi kwa hoja kuwa wamekaa kwa muda mrefu
kwenye foleni kutokana na kitendo cha baadhi yao kununua tiketi nyingi,
hivyo mtu mmoja kuhudumiwa kwa muda mrefu.
“Yaani hawa wauza tiketi ‘sio’ bwana, wanamuuzia mtu mmoja karibu
tiketi za 500,000, hivyo wengine kugandishwa muda mrefu kwenye foleni,
huu sio ustaarabu kabisa, ndio maana wenye hasira wakataka kumvaa hadi
kubomoa mlango wa gari,” alisema kwa hasira mmoja wa mashabiki.
MATOKEO TANGU 2010
APRILI 18, 2010:
Simba 4, Yanga 3: Wafungaji wa Simba walikuwa Uhuru Suleiman (dk 3),
Mussa Mgosi (dk 53 na 74) na Hillary Echesa dakika ya 90. Mabao ya
Yanga yalitoka kwa Athuman Iddi (dk 30) na Jerry Tegete aliyefunga
mawili dk 69 na 89.
Oktoba 16, 2010: Yanga ilishinda bao 1-0, likifungwa na Jerry Tegete dakika ya 70
Machi 5, 2011: Simba na Yanga zilitoka sare ya bao 1-1; bao la Yanga
likifungwa na Stefano Mwasyika kwa penalti dk ya 59 kabla ya Mussa
Mgosi kuisawazishia Simba dk ya 73.
Mei 6, 2012: Simba 5, Yanga 0: Mechi hiyo ya mwisho katika msimu wa
2011/12 iliyochezeshwa na mwamuzi Hashim Abdallah, mabao ya Simba
yalifungwa na Emmanuel Okwi (sekunde ya 10) kabla ya kufunga mengine
mawili dakika ya 62 na 66. Felix Sunzu alifunga dk ya 53 kabla ya
Patrick Mafisango.
Oktoba 3, 2012: Yanga 1, Simba 1. Simba walitangulia kupata bao dakika ya 4, likifungwa na Amri Kiemba.
Ligi hiyo itaendelea pia kwenye viwanja vingine sita kwa Mgambo
Shooting kuwa wenyeji wa African Lyon kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga
huku JKT Ruvu ikiwakaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Chamazi,
jijini Dar es Salaam.
Kipute kingine cha kufunga ligi hiyo, kitakuwa kwenye Uwanja wa
Kumbukumbu ya Sokoine, jijini Mbeya kwa Tanzania Prisons kuwavaa Kagera
Sugar; Oljoro JKT itakuwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid
kuwakaribisha Azam.
Kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro, Polisi Morogoro itakuwa
mwenyeji wa Coastal Union ya Tanga huku Toto Africa ya Mwanza
ikiwakaribisha Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini
Mwanza.
No comments:
Post a Comment